DSC01698
Waumini wa Dini ya Kiislamuwakifuatilia mawaidha.
Na MOblog Team
Waumini wa Kiislamu nchini  wamehaswa kuzingatia maadili kwa kufanya matendo mema katika jamii, kwa kipindi chote watakachokuwa kwenye funga ya  Mwezi Mtukufu wa Ramadhan na baada ya kuisha kwa mwezi huo.
Akitoa mawaidha hayo jijini Dar es Salaam  baada ya kumalizika kwa swala ya Ijumaa wiki ya kwanza ya mfungo mwaka huu, Imam wa Msikiti wa Mtambani Suleiman Abdallah alisema , Uislam ni dini ya amani hivyo ili mja aweze kuwa karibu na Muumba wake anatakiwa kuzidisha ibada na kufanya mambo yaliyo mema hasa kwenye mwezi wa Ramadhani.“Mwezi huu sio mrefu, tumeweza kufanya mambo yetu kwa kipindi chote kwanini tusivumilie katika nyakati fupi ambayo inamfanya mja kuwa daraja la juu kiimani, inatakiwa kuyakimbia mambo ya kipuuzi yasiyokuwa na faida mbele ya Allah,  kwa kufanya ibada na kutekeleza funga kama inavyotakiwa, tunatakiwa kuzidisha ibada, tuwe na subira, utiifu,  nidhamu pamoja na kuzidisha imani yetu kwa muda wote”

Imamu alieleza kuwa, watu wengi wamekuwa wakivutiwa na mambo yanayopoteza wakati na yasiyo na mazingatio wala manufaa katika maisha yao, hali ya kuwa wakiacha kufanya matendo mema yanayompendeza Mwenyezi Mungu.
“Kuna mazingatio makubwa yanayopatikana ndani ya Mwezi Mtukufu, kama kuongeza imani zetu na kupata faradhi mbalimbali zitakazoongeza swawabu kwa matendo tunayoyafanya, pia kuna tahadhari kwa waislamu tunakiwa kuepukana nayo kama kuchanganya ibada na mambo yasiyokuwa na faida kama kufuatilia mpira na mambo mengine yanayoweza kuaribu funga zetu wakati tukiwa   na  swaum”.
Aliongezea kuwa “Watu wanatakiwa kujikita zaidi kwenye ibada, kwani tunafunga mwezi kwa mwaka tena ni siku chache hivyo watu wanatakiwa kuwa wavumilivu ni kipindi kifupi cha mpito, lakini utakuta watu wanaingia uvivu hatimaye mwezi unaisha bila ya kufanya ibada zozote muhimu”