SERIKALI YADHAMIRIA KUKABILIANA KWA VITENDO NA CHANGAMOTO YA KUTOTUMIA FURSA



Na Mwandishi wetu, Pwani

Serikali imesema imedhamiria kukabiliana kwa vitendo na changamoto ya kutotumia fursa na nafasi ya kijiografia ya nchi ya Tanzania na kuifanya kuwa shindani na hivyo kuleta maendeleo endelevu na ustawi wa jamii.

Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe amesema jana mkoani Pwani kuwa hakuna sababu inayoifanya Tanzania isiwe taifa shindani kibiashara katika ukanda huu wa Afrika kutokana na nafasi yake kijiografia miongoni mwa sababu nyingine.

Katika kuonyesha dhamira hiyo kivitendo, Waziri huyo anaongoza ujumbe wa maafisa mbalimbali wa serikali katika kukagua njia kuu toka jijini Dar es Salaam-Tunduma hadi katika mji wa Lubumbashi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Barabara hiyo kuu ndiyo inayotumiwa na magari ya mizigo ya wafanyabiashara wa DRC toka bandari ya Dar es Salaam, hivyo kwa kukagua maeneo ya mizani, serikali inataka kuondoa kero zinazowakumba wafanyabiashara hao.

“Tanzania imebarikiwa kuzungukwa na nchi sita zisizo na bahari na tuna ukanda wa bahari wenye urefu zaidi ya kilometa 1500…lazima tutumie bahati hii kujiletea maendeleo,” aliwaambia waandishi wa habari mara baada ya kutembelea kituo cha kupimia magari cha Maili Moja, Kibaha, mkoani Pwani.

Ziara ya ujumbe huo ilianzia katika bandari ya Dar es Salaam ambapo Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Mhandisi Madeni Kipande ulitoa taarifa fupi kwa Waziri huyo kuhusiana na shughuli bandarini hapo.



Pia ujumbe ulitembelea Kitengo cha kupakia na kupakua kontena (TICS) bandarini hapo.  Maeneo mengine yaliyotembelewa ni pamoja na bandari za nchi kavu (ICDs) maeneo ya Kurasini ambapo Waziri alishuhudia msongamano mkubwa wa malori ya mizigo katika njia hiyo. “Tunataka kubadilika, lazima tubadilike,” alisema Waziri Mwakyembe.



Ujumbe huo unaosafiri kwa barabara ili kupata taarifa za moja kwa moja toka kwa wahusika, unajumuisha pia Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Bw. PeterSerukamba pamoja na mjumbe wa kamati hiyo, Bi. Zarina Madabida.


Akiongea baada ya kukagua kituo cha mizani cha Mikese, Bw. Serukamba alisema wanataka kuangalia na kufahamu kila tatizo kwa kina ili hatimae ufumbuzi wa kudumu upatikane. “Tuko katika ushindani mkubwa, lazima kama nchi tubadilike kwa haraka,” alisema Mwenyekiti huyo wa kamati.

Kwa upande wake, akitoa mfano wa kasoro zilizopo katika vituo vya kupima mizigo alisema bado muda unaotumika kushughulikia gari moja ni mrefu na hivyo kupunguza ufanisi. Waziri Mwakyembe alisema kasoro hizo pamoja na nyingine zitapatiwa ufumbuzi hivi karibuni kutokana na mikakati iliyopo.

Ziara hiyo ya kikazi ya zaidi ya kilometa 2,000 itahitimishwa kwa kufunguliwa kwa ofisi ya TPA Alhamis wiki hii katika mji wa Lubumbashi ambayo ni moja ya mikakati ya kuongeza ufanisi wa bandari katika kuhudumia nchi jirani.

Pamoja na maafisa wengine, ujumbe huo unajumuisha pia maafisa waandamizi toka TPA na Mamlaka ya Usafiri wan chi kavu na Majini (SUMATRA).

Takwimu za hivi karibuni zinaonyesha kuwa shehena yote ya mizigo ya nchi 6 zitumiazo bandari ya Dar es salaam, (yaani Zambia, D R Congo, Burundi, Rwanda, Malawi na Uganda) imeongezeka kutoka tani millioni 3.55 mwaka 2011/12 hadi kufikia tani millioni 4.05 mwaka 2102/13, hiyo ikiwa ni ongezeko la asilimia 14.2.

0 comments:

Copyright © 2013. MSANGIBIN ALLY - All Rights Reserved
Customized by: MSANGIYUSUPHALY | Powered by: KIINICHAHABARI
Designed by: http://kiinichahabaribongo1.blogspot.com/