MEGAWATI 150 KUONGEZEKA KATIKA GRIDI YA TAIFA
Naibu
Mkurugenzi Mtendaji, Uwekezaji Mhandisi Decklan Mhaiki (katikati)
akimweleza Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo
(kushoto) pamoja na Waandishi wa habari moja ya mashine za kufua Umeme
zitakazofungwa katika eneo la Kinyerezi I jijini, Dar es Salaam. Kulia
ni Mkurugenzi Mkazi wa Mradi wa ujenzi huo, Bw. Shaun Moore.
Mmoja
wa mitambo ya kufua umeme ambao utafungwa katika eneo la Kinyerezi I
mara baada ya ujenzi kukamilika. Mitambo hiyo, inatarajiwa kuzalisha
kiasi cha megawati za umeme 150 ambazo zitaunganishwa katika gridi ya
Taifa.
Waziri
wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo katika picha ya pamoja na
baadhi ya watendaji kutoka TANESCO, Wizara ya Nishati na Madini na
watumishi wa kampuni inayojenga kituo hicho ya Jacobsen Elektro.
Waziri
wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo akimsikiliza Mkurugenzi
Mkazi wa Mradi wa ujenzi wa kituo cha Kinyerezi I, Bw. Shaun Moore,
wakati akimweleza maendeleo ya ujenzi wa kituo hicho.
……………………………………………………………………………………..
Na Asteria Muhozya na Jema Marko, Dar es Salaam
Megawati
150 zinatarajiwa kuongezeka katika gridi ya Taifa mara baada ya
kukamilika kwa ujenzi wa mitambo ya kufua umeme eneo la Kinyerezi I
pamoja na kukamilika kwa ufungaji wa mitambo hiyo, ambapo shughuli zima
inatarajiwa kukamilika kabla ya mwezi Disemba mwaka 2014.
Waziri
wa Nishati na Madini Sospeter Muhongo wakati akikagua maendeleo ya
ujenzi wa kituo hicho alieleza kuwa kukamilika kwa ujenzi wa kituo
hicho ni hatua mojawapo ya kutimiza azma ya Serikali ya kuongeza
umeme katika gridi ya Taifa.
Aidha,
aliwataka watanzania na wateja wa umeme kujenga imani na Shirika la
Umeme Tanzania kutokana na mabadiliko ambayo tayari yamefanyika katika
shirika hilo ikiwemo utekelezaji wa mipango mbalimbali ya kuhakikisha
kunakuwa na umeme wa uhakika.
“Nataka
Watanzania muelewe kuwa, Tanesco ya sasa sio kama ya zamani. Umeme
utapatikana. Kampuni ya Jacobsen Elektro ambao wanafanya kazi ya ujenzi
ni wazoefu katika shughuli hizi, tuna imani kazi itakwenda vizuri kama
tulivyopanga. Tanesco itatatua tatizo la umeme”. Alisema Waziri Muhongo.
Katika
hatua nyingine, Profesa Muhongo alieleza kuwa, asilimia 98 ya kampuni
za kitanzania kupata kandarasi katika ujenzi huo ni fursa mojawapo
ambazo watanzania wanatakiwa kuzitumia katika kipindi hiki ambacho nchi
inaingia katika uchumi wa gesi.
Akizungumzia
kuhusu fedha za ujenzi wa kituo cha kinyerezi I na ujenzi wa vituo
vingine vya kinyerezi II, III na IV, Waziri Sospter Muhongo alieleza
kuwa, fedha za ujenzi wa kituo cha Kinyerezi I zimetolewa na Serikali
kupitia TANESCO. Ujenzi wa kituo cha kinyerezi II fedha itatokana na
ubia kati ya Serikali ya Tanzania na Japani , wakati ujenzi wa kinyerezi
III na IV fedha zitatokana na kuingia ubia kati ya Serikali na kampuni
ya Kichina.
Wakati
huo huo, Naibu Mkurugenzi Mtendaji, Uwekezaji, wa Shirika la Umeme
Tanzania (TANESCO) Mhandisi Decklan Mhaiki, aliongeza kuwa, katika kituo
hicho zitafungwa jenereta nne ambapo kila moja itakuwa na uwezo wa
kuzalisha kiasi cha megawati 37.5, hivyo kufanya jumla ya megawati 150
kutoka kituo hicho.
Vilevile,
alieleza kuwa, katika jitihada za kuhakikisha kwamba Shirika la Umeme
Tanzania (Tanesco) linatatua tatizo la Umeme nchini, tayari shirika hilo
na mkandarasi anayejenga kituo hicho, kampuni ya Jacobsen Elektro
wameanza mazungumzo ili kuongeza kiasi kingine cha megawati 200 ili
kituo cha kinyerezi I kiweze kuzalisha umeme wa kiasi cha megawati 350.
Akielezea
kuhusu ubora wa jenereta zitakazofungwa kituoni hapo, Mhaiki alieleza
kuwa, generator hizo ni za kisasa na hazina athari za kimazingira
ikiwemo kelele.
Kwa
upande wake Mkurugenzi Mkazi wa Mradi huo kutoka kampuni ya Jacobsen
Elektro, Bw. Shaun Moore, akielezea maendeleo ya ujenzi wa kituo hicho,
alieleza kuwa, ujenzi wa kituo hicho unaendelea vizuri kutokana na
kampuni hiyo kufanya kazi kwa ushirikiano mzuri na kampuni za kitanzania
zilizochukua kandarasi tofauti tofauti za ujenzi wa kituo hicho, ambapo
takriban asilimia 98 ya kandarasi na wafanyakazi ni kutoka kampuni za
kitanzania.
0 comments: