KUTANA NA MTOTO WA KWANZA KUZALIWA KWA NJIA YA UPANDIKIZAJI NCHINI
Unapoingia
katika nyumba ya familia ya Salehe Saidi, macho na masikio yako
hayawezi kukwepa ucheshi wa kijana wa miaka 13, Jumbe Salehe. Ni kijana
anayeipa tabasamu familia hiyo.
Jumbe ni
mwenye nguvu, afya, akili darasani na uchangamfu ambao kila mzazi
angependa kuuona kwa kijana wake. Lakini Jumbe Salehe, hakuzaliwa kama
watoto wengine. Alipatikanaji katika mchakato mrefu, uliohusisha
teknolojia ya hali ya juu na majaribio yaliyohitaji werevu. Jumbe
alizaliwa kwa njia ya upandikizaji wa mbegu ambao kwa jina la kitaalamu
unajulikana kama In-Vitro Fertilization (IVF). Mchakato huo ulisimamiwa
na Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Wanawake, Profesa Malise Kaisi.
Kwa nini Jumbe alizaliwa kwa njia ya IVF?
Mwanaidi Kombo, mama mzazi wa Jumbe, hakuwa na tatizo la uzazi hapo awali. Alifanikiwa kupata mtoto wake wa kwanza mwaka 1986.
Mwaka
1988 alipata ujauzito mwingine lakini kwa bahati mbaya, uliharibika na
kuanzia hapo ikawa ni vigumu kwake kushika mimba nyingine.
Kutokana
na maumivu hayo, alianza kusaka msaada wa kitabibu na alishauriwa kwenda
kwa daktari wa magonjwa ya wanawake, Dk. Malikiti wa Hospitali ya MM.
Safari
yake kwenda kwa daktari ilimsaidia kung’amua ukweli, kwani aliambiwa
kuwa ana uvimbe mkubwa kwenye kizazi ambao unaweza kuhatarisha maisha
yake na kuwa ndicho chanzo cha kushindwa kupata mtoto.
Hata hivyo, Dk. Malikiti alimuelekeza aende kuonana na Profesa Kaisi kwa kuwa ndiye mtaalamu wa masuala ya uzazi kwa wanawake.
“Nilipofika
kwa Dk. Kaisi, nilimshangaa baada ya kuisoma picha ya Xray. Aliniambia
niache kabisa kunywa dawa nilizoandikiwa za maumivu na kuambia ninywe
panadol endapo nitakuwa na maumivu,” anasema.
Ingawa Mwanaidi alishangaa, aliendelea na kliniki ya Dk. Kaisi akihudhuria kila wiki kwa zaidi ya miezi miwili.
Siku moja
Dk. Kaisi akaamua kumfanyia kipimo cha CT Scan kuangalia mirija ya
uzazi na ndipo alibaini kuwa pamoja na uvimbe, mrija wake mmoja
umepinda.
“Aliniambia
niende nyumbani na nirudi baada ya mwezi mmoja kwa ajili ya upasuaji,
lakini wakati huo alinipa masharti mengi kama nisinywe kabisa chai,”
anasema.
Baada ya
mwezi mmoja, Mwanaidi alirudi kwa Dk. Kaisi ambaye alimwambia ni lazima
amfanyie upasuaji mdogo kwanza kwa ajili ya kurekebisha mirija ya
uzazi.
Katika
upasuaji huo, ambao kitaalamu unaitwa ‘ovary re-implantation’, madaktari
walirekebisha mirija hiyo kwa kufunga kifaa maalumu.
Mwezi
mmoja baadaye Mwanaidi alirudi kwa daktari ambaye aligundua kuwa bado
mwanamke huyo ana uwezo mkubwa wa kuzaa kwani alikuwa na mayai ya
kutosha kumuwezesha kushika ujauzito.
“Aliniambia
nina mayai ya kutosha, lakini tatizo ni hilo la uvimbe na kupinda kwa
mirija ya kusafirisha mayai ya uzazi na mbegu,” anasema.
Baada ya
hapo, Mwanaidi alifanyiwa upasuaji mwingine mkubwa kwa ajili ya kuondoa
uvimbe. Zoezi hilo lilifanikiwa kwa kiasi kikubwa ingawa siyo kuondolewa
kizazi.
Baada ya
hatua hii, Profesa Kaisi alimshauri Mwanaidi kuendelea kutafuta mtoto
mwingine kwa sababu anao uwezo wa kubeba mimba ingawa itakuwa vigumu kwa
yeye kupata ujauzito huo kwa njia ya kawaida.
Profesa
Kaisi anasema aliwashauri kuwa wanaweza kupata ujauzito kwa njia ya
upandikizaji jambo ambalo lilikubaliwa mara moja na wazazi hao. Disemba
2012, Mwanaidi alifanikiwa kushika ujauzito kwa njia ya IVF.
Iliwezekana baada ya mbegu za mume wake na mayai yake (Mwanaidi)
yaliyopevushwa, kutolewa na baadaye kupandikizwa katika nyumba ya uzazi
ya Mwanaidi.
“Baada ya
mchakato huo kumalizika nilitakiwa kuhudhuria kliniki kila wiki kwa
ajili ya kuangaliwa jinsi mimba inavyokua,” anasema Mwanaidi.
Mwanaidi
anasema katika ujauzito ule hakuwa akiumwa au kupata matatizo yoyote
kama ilivyokuwa kwenye ujauzito wake wa kwanza. Alikuwa na hali ya
kawaida kabisa kuliko alivyotarajia.
Anasema
Profesa Kaisi alimwambia kuwa huenda angejifungua Agosti 17, mwaka 2000
na ikawa hivyo. Alijifungua siku hiyo saa 2:00 usiku kwa njia ya
upasuaji.
“Namshukuru
Mungu kuliko kawaida. Huu kwangu ni muujiza na ninamshukuru sana
Profesa Kaisi kwa uwezo ambao Mungu amempa,” anasema Mwanaidi.
Mwananidi anamwelezea mtoto wake kuwa ni mwenye nguvu, mwili mkubwa, na mcheshi.
“Ni mtoto
wa kawaida kabisa, ana uwezo mkubwa darasani na alifaulu vizuri mtihani
wa darasa la saba. Ni mtoto mwenye kumbukumbu za ajabu,” anasema mama
huyo wa Jumbe.
Mwanaidi
anasema kwa kuwa sasa ana watoto wawili, bado anatamani mtoto mwingine
na anasema iwapo Profesa Kaisi angekuwa hajapooza, angeomba apate mtoto
mwingine kwa njia ya IVF.
“Kuugua
kwa Prof. Kaisi ni pigo kwa kila mtu. Wapo mamia ya wanawake wanaohitaji
huduma za uzazi... kwa kweli sijui itakuwaje,” anasema.
Si hivyo
tu. Mwanaidi anasema Profesa Kaisi hakuwahi kuwalipisha hata senti tano
ya matibabu tangu alipofanyiwa upasuaji wa uvimbe hadi alipopata
ujauzito kwa njia ya IVF.
Profesa
Kaisi anasema hakuweza kuwalipisha fedha katika mchakato huo kwa sababu
matibabu hayo yalikuwa chini ya programu iliyodhaminiwa na watu kutoka
nje, ambao walilipia gharama zote.
IVF hufanyikaje?
Profesa
Kaisi anasema yai la mama hupevushwa kwa kutumia dawa maalumu na
hufuatiliwa kwa kutumia mashine ya uchunguzi wa ndani ya
mwili(Ultrasound).
“Baada ya
yai kukomaa, sindano maalum yenye wembamba mithili ya unywele huingizwa
ukeni hadi kwenye mirija na yai lililopevuka huchukuliwa na kutolewa
nje,” anasema.
Yai au
mayai hayo huwekwa kwenye chombo maalumu (test tube) kabla ya
kuhamishwa kwenye beseni maalumu ambalo hufanya yai liendelee kuwa hai
licha ya kutoka nje ya mwili wa binadamu.
“Beseni
hilo halina budi kuwa na mazingira kama ya mwilini. Kwa mfano joto,
mwanga na kusiwepo na sauti, kwani yai huweza kuharibika kwa kasoro
ndogo ndogo sana,” anasema.
Anasema
wakati huo mbegu za mwanaume hupimwa kama hazina walakini na hutolewa
kwa mwanaume kujichua au kama hawezi kujichua basi hutakiwa kufanya
tendo la ndoa na mke wake na kisha mbegu kukingwa kabla ya kuwekwa
kwenye chombo maalumu.
Mbegu za baba hutakiwa kutolewa saa mbili mara tu baada ya yai la mama kutolewa ili visipishane.
“Baada ya
yai na mbegu kutolewa, hatua inayofuata ni kuichoma mbegu kwenye yai
kwa kutumia sindano maalumu. Mchakato huu unaitwa kwa kitaalamu, Intra
Cytoplasmic Sperm Injection au ICSI),” anasema.
Anaeleza
kuwa, baada ya mbegu na yai kuchanganywa, huwekwa kwenye chombo maalumu
cha joto kitaalamu ‘Incubator” kwa saa 40 kabla ya kuwekwa au
kupandikizwa kwenye kizazi cha mama.
“Hali
kadhalika ‘incubator’ inatakiwa kuiga hali ya tumboni mwa mama wakati
yai la mama na mbegu za baba vinapowekwa kabla ya kuwekwa kwenye kizazi
cha mama, kwa mfano joto, mwanga na sauti,” anasema Profesa Kaisi.
0 comments: