TAARIFA MBALIMBALI ZA KIMICHEZO KUTOKA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TFF
WANG’AMUZI VIPAJI MABORESHO STARS WAJICHIMBIA LUSHOTO
Wang’amuzi
vipaji 28 wanakutana Lushoto mkoani Tanga kwa siku saba katika mpango
maalumu wa maboresho ya Taifa Stars ambapo watatoka na orodha ya mwisho
ya wachezaji waliopatikana katika mechi za maboresho hayo zilizochezwa
nchi nzima.
Katika
kikao hicho, wang’amuzi hao watapitia majina ya wachezaji walioteuliwa
ikiwemo kuwaangalia tena kwenye video kwa vile mechi zote zilirekodiwa.
Wachezaji watakaoteuliwa katika mpango huo baadaye wataingia kambini
mkoani Mbeya.
Wang’amuzi
vipaji ambao wanaoondoka Machi 9 mwaka huu kwenda Lushoto ni Abdul
Mingange, Boniface Pawasa, Charles Mkwassa, Dan Korosso, Dk. Mshindo
Msolla, Edward Hiza, Elly Mzozo, Hafidh Badru, Hamimu Mawazo, John
Simkoko, Jonas Tiboroha, Juma Mgunda na Juma Mwambusi.
Kanali
mstaafu Idd Kipingu, Kenny Mwaisabula, Madaraka Bendera, Madaraka
Selemani, Mbarouk Nyenga, Mohamed Ally, Mussa Kissoky, Nicholas Mihayo,
Peter Mhina, Salum Mayanga, Salvatory Edward, Sebastian Nkoma, Sekilojo
Chambua, Selemani Jabir na Shabani Ramadhan.
Wengine
ni Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF ambaye pia ni Mwenyekiti wa
Kamati ya Ufundi, Kidao Wilfred, Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF
ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Vijana, Ayoub Nyenzi, Kaimu
Mkurugenzi wa Ufundi, Salum Madadi na Mshauri wa Rais (Ufundi),
Pelegrinius Rutayuga.
MUJUNI KUICHEZESHA AFC LEOPARDS CC
Mwamuzi
Israel Mujuni ameteuliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu (CAF)
kuchezesha mechi ya marudiano ya Kombe la Shirikisho (CC) Afrika kati ya
wenyeji AFC Leopards ys Kenya na SuperSport United ya Afrika Kusini.
Mujuni
katika mechi hiyo itakayochezwa kesho (Machi 8 mwaka huu) jijini
Nairobi, Kenya atasaidiwa na Samuel Mpenzu, Josepht Bulali wakati
mwamuzi wa mezani atakuwa Ramadhan Ibada.
Kamishna
wa mechi hiyo ni Amir Hassan kutoka Mogadishu, Somalia. SuperSport
United ilishinda mechi ya kwanza iliyochezwa wiki mbili zilizopita mabao
2-0.
SIMBA YALIMWA FAINI KWA KUENDEKEZA VITENDO VYA KUSHIRIKINA
Bodi
ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) imeipiga faini ya jumla ya sh. milioni moja
klabu ya Simba kutokana na makosa mbalimbali ikiwemo vitendo
vinavyoashiria ushirikina uwanjani.
Simba
ilifanya vitendo hivyo katika mechi yake dhidi ya Mbeya City ambapo
imepigwa faini ya sh. 500,000. Pia imepigwa faini nyingine ya sh.
500,000 kwa makocha wake Loga, Selemani Matola na Idd Pazi kuingia
uwanjani na kumzonga mwamuzi kwenye mechi hiyo.
Naye
mshambuliaji wa Simba, Amisi Tambwe amepigwa faini ya sh. 500,000 kwa
kushangilia bao alilofunga kwenye mechi hiyo kwa kuonesha ishara ya
matusi kwa kidole.
Mbeya
City imepigwa faini ya sh. 300,000 kwa washabiki wake kuingia uwanjani
kwenye mechi dhidi ya Kagera Sugar iliyochezwa mjini Bukoba. Klabu za
Yanga na Coastal Union zimepigwa faini ya sh. 500,000 kila moja kwa
washabiki wao kurusha chupa za maji uwanjani wakati timu hizo
zilipopambana jijini Tanga.
Kiungo
wa Mtibwa Sugar, Shabani Nditi amepigwa faini ya sh. 500,000 kwa
kumpiga mchezaji wa Simba, wakati Salvatory Ntebe pia wa Mtibwa Sugar
amepigwa faini ya sh. 500,000 kwa kumtukana refa kwenye mechi dhidi ya
Mbeya City.
Pia
mshambuliaji wa Mtibwa Sugar, Musa Mgosi amepigwa faini ya sh. 500,000
kwa kosa la kupiga uwanjani kwenye mechi dhidi ya Ashanti United ambapo
vilevile atakosa mechi tatu za ligi. Coastal Union imepigwa faini ya sh.
500,000 kwa washabiki wake kumrushia chupa za maji kipa wa Mbeya City.
Nayo
JKT Ruvu imepigwa faini ya sh. 300,000 kwa kuchelewa kufika uwanjani
kwenye mechi dhidi ya Simba iliyochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Vilevile
wamiliki wa Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga wameandikiwa barua ya
kufanya marekebisho ya vyumba vya wachezaji, kwa vile havina hewa ya
kutosha.
Kwa
upande wa Ligi Daraja la Kwanza (FDL) klabu zilizopigwa faini kutokana
na makosa mbalimbali ni Friends Rangers (sh. 200,000), Lipuli (sh.
200,000), Majimaji (sh. 400,000), Polisi Morogoro (sh. 400,000) na
Transit Camp (sh. 200,000).
Kocha
Msaidizi wa Polisi Morogoro, John Tamba atapelekwa kwenye Kamati ya
Maadili kutokana na vitendo visivyo vya kimaadili katika mechi dhidi ya
Burkina Faso.
Kiongozi
wa Lipuli, Hamis Kiemba na wachezaji Boniface Sawaka, George Enock na
Green Paul watapelekwa katika Kamati ya Nidhamu kutokana na utovu wa
nidhamu waliofanya kwenye mechi dhidi ya Kimondo.
Naye
mchezaji Sangalau Nyamoka wa JKT Kanembwa aliyelalamikiwa uhalali wake
na Polisi Tabora suala lake linapelekwa Kamati ya Nidhamu.
COASTAL, ASHANTI KUUMANA MKWAKWANI VPL
Ligi
Kuu ya Vodacom (VPL) inaendelea kesho (Machi 8 mwaka huu) kwa mechi
tatu ambapo Coastal Union itaumana na Ashanti United kwenye Uwanja wa
Mkwakwani jijini Tanga.
Ruvu
Shooting itaikaribisha Oljoro JKT kwenye Uwanja wa Mabatini, Mlandizi
mkoani Pwania wakati Mbeya City itacheza na Rhino Rangers kwenye Uwanja
wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya.
Mechi
za Jumapili (Machi 9 mwaka huu) ni Tanzania Prisons na Simba kwenye
Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya, na JKT Ruvu na Mtibwa
Sugar zitacheza Uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi, Dar es Salaam.
FDL KUTIMUA VUMBI WIKIENDI
Ligi
Daraja la Kwanza (FDL) inaendelea wikiendi hii kwa timu za makundi yote
matatu kushuka kwenye viwanja tofauti nchini ambapo kesho (Machi 8
mwaka huu) Tessema itacheza na Transit Camp kwenye Uwanja wa Karume, Dar
es Salaam.
Kundi
B ni Burkina Faso vs Kurugenzi (Jamhuri, Morogoro) wakati C Polisi
Tabora vs Mwadui (Ali Hassan Mwinyi), Stand United vs Pamba (Kambarage),
Polisi Mara vs Kanembwa JKT (Karume) na Polisi Dodoma vs Toto Africans
(Jamhuri, Morogoro).
Mechi
za Jumapili ni kundi A, African Lyon vs Polisi Dar (Karume), Villa
Squad vs Friends Rangers (Mabatini, Pwani) na Ndanda vs Green Warriors
(Nangwanda Sijaona, Mtwara). Kundi B ni Polisi Morogoro vs Majimaji
(Jamhuri, Morogoro) na Mlale JKT vs Lipuli (Majimaji, Songea).
0 comments: