WAZIRI WA JK ATONESHA KIDONDA NDANI YA CCM. SOMAA HIII KUJUA KISA NN HAPAAA


Bernard Membe.

HALI ya kisiasa ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) imezidi kupandisha joto, baada ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe kutumia nafasi ya kuzindua filamu ya I Love Mwanza kujinadi kisiasa.

Membe ni miongoni mwa makada sita wa CCM waliopewa onyo kali kutokana na kukiuka miiko ya chama pamoja na kuanza kampeni kabla ya wakati.

Wakati hali ikiwa hivyo, Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Nape Nnauye, ameyakana maneno yake aliyoyatoa Februari 19, mwaka huu kuhusu uamuzi wa chama kuwapa adhabu ya kuwafungia kwa kipindi cha mwaka mmoja makada sita wa chama hicho.

Membe alisema kitu alichokifanya kina baraka zote za Rais Jakaya Kikwete.

Viongozi waliotiwa hatiani ni Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe.

Wengine ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Stephen Wassira, Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba na aliyewahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja.

Akiwa jijini Mwanza mwishoni mwa wiki iliyopita alipokuwa akizindua filamu inayoitwa I Love Mwanza, Membe alisema maneno yanayohusishwa na kufanya kampeni za urais.

“Kabla sijaja Mwanza nilikwenda kwa Rais Jakaya Kikwete kumuaga na kumueleza kusudio langu la kuja kufanya shughuli hii naye akanikubalia na kunipa baraka zote.

“Rais aliponikubalia alinitaka nije huku haraka na nisiache na baada ya kurudi jijini Dar es Salaam nikampatie taarifa za kile nilichokishuhudia jijini hapa.

Hapa siko peke yangu, nimekuja na marafiki zangu wapendwa wanaoitwa Friends of Membe,” alisema Membe.

Kati ya watu waliokuwa wamefuatana na Membe ni pamoja na Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, aliyesema: “Rafiki yangu huyu nampenda sana na ni tarajio jipya kwa Watanzania…, kwa hiyo tumuunge mkono mimi nina imani naye, iko siku moja atakuwa kiongozi mkubwa wa taifa hili.”

Ikulu
Katibu Mkuu Kiongozi, Ombeni Sefue akizungumza na gazeti hili jana, alisema hawezi kuzungumza chochote juu ya kile alichokisema Membe kwa kuwa yeye hakuwepo na hajasikia.

Kuhusu Rais kumtuma Membe, Sefue alisema hawezi kuthibitisha hilo, kwani hana taarifa na siyo lazima kila Rais anapotuma watu wake yeye ajue.

“Siyo lazima kila Rais anapowatuma mawaziri wake nijue na sishangai kama alimtuma ila kwa kweli siwezi kusema chochote,” alisema Balozi Sefue.

Alichosema Februari 19
Nnauye akizungumza na waandishi wa habari Februari 19 mwaka huu, alisema wanachama sita walitiwa hatiani kwa makosa ya kuanza kampeni za kuusaka urais wa 2015 kabla ya wakati, jambo ambalo ni kinyume cha taratibu za chama hicho, hivyo kutoa onyo kali.

Adhabu ya onyo kali kwa mujibu wa taratibu za chama hicho inamaanisha kuwaweka chini ya uangalizi kwa miezi 12 ili kuhakikisha hawajihusishi na vitendo vyovyote vinavyokwenda kinyume na misingi ya chama hicho, vinginevyo hatua kali zitachukuliwa dhidi yao.

“Mwanachama aliyepewa onyo kali atakuwa katika hali ya kuchunguzwa kwa muda usiopungua miezi 12 ili kumsaidia katika jitihada zake za kujirekebisha,” alisema Nnauye.

Hatua hiyo ya CCM imezitia doa harakati za vigogo hao, kwani watatumikia adhabu yao hadi Februari 2015 na wakati wote watakuwa wakichunguzwa mienendo yao.

Alisema makada hao kwa kuanza kwao kampeni za kutafuta kuteuliwa kuwania urais kabla ya wakati ni kinyume na kanuni za uongozi na maadili za CCM, toleo la Februari 2010, Ibara 6 (7)(i).

“Wamethibitika kufanya vitendo vinavyokiuka maadili ndani ya chama na baadhi yao kufanya vitendo vinavyokiuka maadili ndani ya jamii. “Vitendo vya namna hii ni kosa kwa mujibu wa kanuni za uongozi na maadili za CCM toleo la Februari 2010, Ibara kadhaa za kanuni hizo,” alisema Nnauye.

Alisema: “Kamati Kuu baada ya kuthibitisha makosa hayo, imewapa watu wote sita waliohojiwa adhabu ya onyo kali na kuwataka wajiepushe na vitendo vinavyokiuka maadili na iwapo wataendelea na vitendo hivyo, chama kitawachukulia hatua kali.”

Alisema Kamati Kuu imeiagiza kamati ya maadili kuwachunguza mawakala na watendaji wa wanachama hao waliokuwa wakiratibu shughuli mbalimbali ili waweze kuchukuliwa hatua kali za kinidhamu, hatua inayolenga kuhakikisha chama hakigawanyiki.

Nnauye alisema ibara 6 (2) (1-5) ya maadili ya viongozi wa chama hicho inawazuia kutoa michango, misaada, zawadi za aina yoyote, kukusanya michango na kufanya kampeni bila ya kupata kibali kutoka kamati ya siasa ya halmashauri ya eneo husika.

Kauli ya Nape jana.
Alipoulizwa kuhusiana na kauli ya Membe, Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye alisema si dhambi bali kinachozuiwa ni matendo yanayohatarisha usalama wa chama.

“Si dhambi mtu kutangaza nia ya kugombea urais, tunasema matendo mabaya yanayohatarisha uhai wa chama ndiyo hatutaki. Unajua hata mie naweza kutangaza kugombea ubunge pale Ubungo si kosa,” alisema Nape.

Malecela na Friends of Lowassa .
Januari 30, Makamu Mwenyekiti Mstaafu wa chama hicho, John Malecela alitaka uongozi wa chama hicho umchukulie hatua Lowassa kwa kile alichosema ni kuanza mapema kampeni.

Katika mkutano wa waandishi wa habari, Malecela alipoulizwa ni kwa nini ameamua kumtaja kwa jina Lowassa pekee huku kukiwa na makada wengi wanaojipitisha kupiga kampeni za urais, kabla ya kujibu, Malecela aliingia ndani ya nyumba yake na kutoka akiwa ameshikilia mfuko uliokuwa na fulana mbili.

Alitoa fulana hizo, moja ikiwa na rangi nyeusi na kahawia na nyingine yenye rangi nyekundu na nyeupe zikiwa zimeandikwa ‘Friends of Edward Lowassa’ (Marafiki wa Edward Lowassa).

“Hivi kuna mwingine aliyefanya hivi? Na hizi zimegawiwa nchi nzima. Ehhh! Hivi kuna mwingine kafanya hivi? Sijui, niongezee nini tena zaidi ya hapo,” alisema Malecela huku akionyesha fulana hizo.

Jana alipotafutwa na MTANZANIA ili kuzungumzia kauli ya Membe ya kusema ameambatana na ‘Friends of Membe’, alisema: “Samahani nipo najiandaa naenda kuweka jiwe la msingi la Nyerere Foundation.” Baada ya maelezo hayo alikata simu.MTANZANIA

0 comments:

Copyright © 2013. MSANGIBIN ALLY - All Rights Reserved
Customized by: MSANGIYUSUPHALY | Powered by: KIINICHAHABARI
Designed by: http://kiinichahabaribongo1.blogspot.com/