WABUNGE WANAOUNDA UKAWA WAREJEA BUNGENI DODOMA.

http://www.thehabari.com/wp-content/uploads/2012/02/Picha-no-1-2.jpgMWENYEKITI wa Chama Cha Kijamii (CCK) na Mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, Constantine Akitanda amesema juhudi zao walizoanzisha na chama cha NRA, zimelenga kuhakikisha kuwa wajumbe wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), wanarejea bungeni.

Aidha, amemtaka Naibu Katibu Mkuu CUF, Julius Mtatiro kuacha kubeza vyama vingine, visivyokuwa na dola kama CCK na NRA, kwani hakuna chama cha siasa kikubwa wala kidogo, vyote viko sawa.

Akitanda alisema hayo Dar es Salaam jana, alipokuwa akifafanua juu ya taarifa iliyotolewa na Mtatiro juzi, kuwa "hawezi kubishana na vyama vidogo vyenye maslahi binafsi."

Mtatiro alitoa kauli hiyo, baada ya kuulizwa na waandishi, juu ya taarifa iliyotolewa na Akitanda na Mwenyekiti wa Taifa wa NRA, Rashid Mtuta, mwishoni mwa wiki kuwa watafanya ziara mikoani kushinikiza Ukawa warejee bungeni na pia kuhakikisha kuwa mchakato wa Katiba mpya unaendelea, ikiwemo mijadala ndani ya Bunge Maalumu la Katiba.

"Hatuwezi kubishana na Mtatiro, ni kijana mdogo sana kiumri na kisiasa na hata kiwadhifa. Ni Naibu Katibu Mkuu tu, kwa hiyo si saizi yetu. Tunaomba ieleweke kuwa imekuwa ni tabia ya baadhi ya wanasiasa na vyama vya siasa, kubeza vyama vingine na kuviita ni vyama vidogo," alisema Akitanda.

Alieleza kuwa sheria ya nchi imeruhusu mfumo wa vyama vingi vya siasa ;na kila mwananchi ana haki ya kutafuta wananchi, ambao wana mtazamo unaofanana kiitikadi na kisera kuungana na kuanzisha chama cha siasa.

Aliongeza "Taratibu za kuanzisha chama zinafahamika na ukitimiza masharti unapata usajili, na ukishapata usajili tayari ni chama cha siasa na hakuna tafsiri wala msamiati wa kuwa hiki ni chama cha siasa kikubwa au kidogo hakuna chama cha siasa jike wala dume."

Alisema kamwe haiwezekani kuwa kutokana na vyama vingine havikushinda dola, basi vishirikiane na vyama vilivyopo katika dola kwa kila jambo, hata kama jambo hilo litaleta maafa kwa Taifa.

Alieleza kuwa hata hao Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi ambao wote wanaunda Ukawa, wanatofautiana katika mambo mengi; na mfano ni Juni 8, mwaka huu Kituo cha Demokrasia Tanzania, yaani Tanzania Centre for Democracy (TCD), kiliitisha mkutano wa viongozi wakuu wanachama wa TCD huko Dodoma. "Chadema na CUF walisusia mkutano huo kwa sababu zao, lakini NCCR-Mageuzi kilihudhuria," alisema Akitanda.

Alisema; “lazima tukubali kuna kutofautiana na kushutumiana. Kwa mfano hao CUF walipofanya jambo jema la kuleta utengamano Zanzibar na kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa; na Maalim Seif Sharif Hamad akawa Makamu wa Kwanza wa Rais, cha kushangaza hao hao maswahiba wao wakubwa, Chadema, waliwaponda na kuwabeza na kukataa kata kata kuunda nao Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, kwa madai CUF si chama cha upinzani tena, kwa sababu wana ndoa na CCM.

"Swali la kujiuliza ni Je? CUF walipounda Serikali ya Umoja wa Kitaifa na CCM huko Zanzibar ilikuwa ni kwa maslahi gani?" Alihoji.HABARILEO


0 comments:

Copyright © 2013. MSANGIBIN ALLY - All Rights Reserved
Customized by: MSANGIYUSUPHALY | Powered by: KIINICHAHABARI
Designed by: http://kiinichahabaribongo1.blogspot.com/