KWA HILI MARCIO MAXIMO UMETISHA, KIROHO SAFI! MAISHA YANATAKIWA KUENDELEA YANGA SC
Mbrazil
Marcio Maximo hakuwa na mahusiano mazuri na Juma Kaseja mwaka 2007
alipokuwa anaifundisha Taifa Stars, lakini sasa amesema kazi inatakiwa
kundelea Yanga kama kawaida na kusahau yaliyopita
Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
0712461976
Imechapishwa Juni 28, 2014, saa 4:38 asubuhi.
KOCHA Mbrazil, Marcio Maximo na msaidizi wake Leonadro Neiva wanatarajia kuanza kazi rasmi jumatatu baada ya kumwanga wino kuitumika Yanga sc kwa mkataba wa miaka miwili.
Jana
Maximo na mwenzake Neiva walikuwa na mkutano na waandishi wa habari
makao makuu ya Yanga, makutano ya Twiga na Jangwani, Kariakoo, jijini
Dar es salaam ambapo walieleza malengo yao na kujibu maswali ya
wanahabari.
Ulikuwa
mkutano mzuri na muhimu kwa wanamichezo, kwasababu walikuwa na kiu ya
kujua nini Maximo ataongea kwa mara ya kwanza baada ya kurudi nchini,
safari hii ikiwa ni Yanga na sio majukumu ya kitaifa.
Moja
ya mambo aliyosema Maximo ni kufurahia kurudi Tanzania, iliwasifu
watanzania kwa kuwa wakarimu, wapenda mpira na akaahidi kufanya kazi kwa
ueledi mkubwa.
Pili
Maximo hakusita kutoa shukurani zake kwa viongozi wa Yanga kwasababu
wamemuamini na kumpa nafasi hiyo muhimu. Alikiri kufuatwa kwa awamu tatu
mfufulizo, lakini safari hii akaona bora akubali.
Kitu
ambacho wengi walisubiri kusikia kutoka kwa Mbrazil huyu mwenye heshima
kubwa nchini, nikiwemo mimi, ni mipango yake ya kuifanya Yanga kuwa
bora.
Maximo
alipata fursa ya kueleza mipango yake ambapo alisema anatarajia kuanza
kazi moja kwa moja siku ya jumatatu pamoja na msaidizi wake Neiva kwa
kushirikiana na kocha wa kikosi cha U-20.
Alisema ataanza na wachezaji waliopo na wachezaji wa kikosi cha U20 ambapo watakua wakifanya mazoezi pamoja.
“Natambua
tuna wachezaji wengi katika timu za Taifa mbalimbali ikiwemo ya
Tanzania (Taifa Stars), Uganda (The Cranes) na Rwanda (Amavubi) ambao
wapo wanayatumikia mataifa yao, na punde watakapomaliza majukumu hayo
wataungana nasi kwa maandalizi”.
Juma Kaseja ataendelea kufanya kazi na Maximo
Alisema
mambo mengi, lakini yote yalilenga kuijenga Yanga mpya. Hakusahau
kuomba uvumilivu kwa wanachama na mashabiki wa Yanga kwasababu soka
linahitaji kwenda kwa namna mbili.
Moja
unaweza kwenda haraka na mipango, lakini njia bora kwa klabu kama Yanga
ni kwenda taratibu kwasababu ina safari ndefu ya kufikia kilele cha
mafanikio.
Maneno ya Maximo yanaenda sambamba na kocha aliyekuwa anaifundisha Taifa stars kabla ya Mart Nooij, Mdenish Kim Poulsen.
Mara nyingi Kim alikuwa anapenda kusema “Things Takes Time” (TTT) . Kwa tafsiri isiyo rasmi, anamaanisha mambo yanahitaji muda.
Kila
jambo linahitaji kupewa muda ili lifanyike vizuri. Walimu wengi wa soka
wanajua hili, soka si jambo la haraka. Hata hao wanaoonekana kuwa bora
duniani, walitumia muda mrefu kujenga soka lao.
Yanga
ni klabu kongwe kiumri, lakini kimafanikio, hasa ngazi ya kimataifa ni
changa. Mipango thabiti inatakiwa kuwekwa, lakini lazima uvumilivu
uwepo.
Maximo
ni mtu wa mipango, ni muumini wa falsafa yake, ana namna ya kufanya
mambo yake, ana msimamo mkali hasa masuala ya nidhamu, hivyo wanachama,
viongozi na wadau wa Yanga wamuamini na kumuacha atekeleze mipango yake
ili siku moja Yanga ifike mbali.
Lakini
yote kwa yote, Maximo alisema mambo mengi muhimu. Kuna watu walisubiri
kuuliza maswali, na moja ya swali nililotegemea kulisikia jana ni kuhusu
Juma Kaseja.
Kaseja ni kipa mkongwe, na wengi wanamuita `Tanzania One`. Kwa miaka takribani 10 aliichezea Simba kwa mafanikio.
Alifanya
kazi nzuri medani ya kitaifa na kimataifa, lakini baadaye viongozi wa
Simba walimtoa kafara na kushindwa kabisa kumuheshimu.
Yalisemwa mengi lakini sababu waliyosema viongozi ni kwamba kipa huyo alikuwa ameshuka kiwango.
Juma
Kaseja alifungwa bao rahisi na Awadh Juma katika mechi ya Nani Mtani
jembe, mwezi desemba mwaka jana, lakini ilikuwa sehemu ya mchezo. Picha
kwa hisani ya Global Publisher.
Kaseja
baada ya kumaliza mkataba wake na Simba msimu wa 2012/2013,
hakuongezewa, na alilazimika kukaa nusu msimu (2013/2014) baada ya
kukosa timu.
Yanga waliokuwa na majukumu ya ligi ya mabingwa barani Afrika, walilazimika kumsajili Kaseja mwenye uzoefu.
Usajili
huo ulizua mengi, lakini mwisho wa siku, viongozi wa Jangwani walisema
uzoefu wa Kaseja ndio umewavutia kumsainisha na atatumika katika
michuano ya kimataifa.
Wakati
Kaseja akisajiliwa kwenda Yanga, nilihofia atapata matatizo kutokana na
hali halisi iliyokuwa imemtokea nyuma na klabu yake ya Simba.
Kitendo cha kuachwa na kushindwa kuheshimika, kilimvuruga Kaseja na kila ukikutana naye alikuwa anaonekana mwenye mawazo.
Kwa
kazi aliyofanya Simba, sidhani kama alitarajia kuachwa kwa namna ile.
Haikuwa haki, ingawa Simba walikuwa na chaguo lao. Hakuna ambaye
angeweza kuwalazimisha kumbakisha kipa huyu aliyewasaidia kuitoa
Zamalek, ligi ya mabingwa mwaka 2003.
Baada
ya kurudi Yanga kwa mara ya pili Kaseja aliidakia klabu hiyo kwenye
mechi ya `Nani Mtani Jembe`. Hii ilikuwa mwezi desemba mwaka jana uwanja
wa Taifa jijini Dar es salaam
Baada
ya kuona kikosi cha kwanza kilichopangwa na aliyekuwa kocha mkuu,
Mholanzi, Ernie Brandts akisaidiwa na Fredy Felix Minziro, niligundua
kuwepo kwa majina mawili muhimu, Juma Kaseja na Emmanuel Okwi.
Hawa
walisubiriwa sana siku hiyo. Yanga walifungwa mabao 3-1, huku bao la
kufutia machozi likifungwa na Okwi aliyekuwa gumzo kwa wakati huo.
Kwa
bahati mbaya sana, Kaseja alifanya kosa moja kubwa lililosababisha
kufungwa goli la kizembe na mshambuliaji wa Simba, Awadh Juma.
Hili lilikuwa bao jepesi na kwa vyovyote vile Kaseja alilazimika kubeba lawama.
Wakati natoka uwanjani, nilipita jukwaa la Yanga, hakika mashabiki waliowengi walilaumu na wengine kusema Kaseja hana lolote.
Kimpira,
kosa la Kaseja lilikuwa la kawaida, hata akina Iker Casillas wanafungwa
mabao kama yake. Si mliona kombe la dunia Casillas akifanya makosa?
Baada
ya tukio lile, ilionekana wanachama na wapenzi wengi wa Yanga wanakosa
imani na Kaseja. Kama kawaida ya Watanzania, wachezaji wanabeba lawama
kubwa wanapofanya makosa uwanjani.
Wengi
wanasahau kuwa mpira ni mchezo wa makosa. Ili ufunge bao lazima
mpinzani wako afanye kosa. Wapi uliona goli linafungwa bila kufanyika
kosa? Yatakuwa maajabu.
Kila goli ni matokeo ya makosa. Kukosea kwa Kaseja ilikuwa kawaida na ni mambo ya mpira.
Kaseja akiwa kazini Yanga sc
Lakini
alipoanza kuichezea Yanga kwenye michuano ya ligi kuu mzunguko wa pili
msimu uliopita, kwa bahati mbaya sana, Kaseja alifanya kosa mwezi machi
mwaka huu kwenye mechi dhidi ya Mtibwa Sugar ndani ya uwanja wa Jamhuri
kwa kufungwa bao jepesi na mechi kumalizika kwa sare ya 1-1.
Mechi
hii ilikuja siku chache baada ya Yanga kutolewa kwa mikwaju ya penati
na National Al Ahly ya Misri katika michuano ya ligi ya mabingwa.
Kaseja alianza katika mechi hii baada ya kipa namba moja, Deo Munish kukatwa mkono wake na bati akiwa nyumbani kwake.
Baada
ya mchezo huo, Kaseja akaendelea kutupiwa lawama, na alipoenda Tanga
kucheza dhidi ya Mgambo ambapo Yanga walifungwa 2-1 na kuanza kupoteza
matumaini ya kutwaa ubingwa, alifungwa bao jepesi kwa mara nyingine.
Mambo yakawa mabaya zaidi, presha kubwa ya mashabiki wa Yanga ilimfanya kaseja apoteze hali ya kujiamini.
Nakumbuka
kwenye mchezo wa Azam dhidi ya Yanga uwanja wa Taifa ambapo timu hizo
zilitoka sare ya 1-1, Kaseja alicheza kwa wasiwasi mkubwa.
Lakini
haya yalitokea kwa Kaseja kama yanavyotokea kwa makipa wengine bora
duniani. Tatizo la mashabiki wengi wa Tanzania wanaangalia mpira wa
ulaya kwa jicho lingine na mpira wa Tanzania.
Ulaya
wachezaji wanakosea na mashabiki wa Tanzania wanaona ni kawaida, lakini
kwetu mtu akifanya kosa kama la Casillas, basi utasikia kauza mechi,
kahujumu…na maneno mengi.
Katika
historia ya Kaseja, kamwe hakuwahi kuwa na uhusiano mzuri na kocha
Maximo wakati huo akiifundisha Taifa stars. Kaseja alikuwa na tatizo na
Maximo mwaka 2007, na nadhani lilianzia katika kipigo cha 4-0 kutoka kwa
Senegal mjini Dakar.
Inasemekana Kaseja aligoma kumbadili Ivo Mapunda aliyekuwa amefungwa bao 4-0 kwa muda mfupi wa kipindi cha pili.
Tangu
hapo Kaseja hakuwahi kuichezea Taifa stars chini ya Maximo. Watu
walishinikiza kuitwa kwa Kaseja, lakini kama nilivyosema, Maximo ni mtu
wa msimamo mkali na anapenda kufanya mambo yake kwa namna yake.
Jana
wengi walitamani kusikia kauli ya Maximo kuhusu Kaseja ambaye anakutana
naye Yanga sc. Wawili hawa wanakwenda kufanya kazi pamoja.
Maximo aliulizwa swali kuhusu Kaseja ambapo alikiri kuwa waliwahi kuwa na matatizo, lakini yale yalishapita.
“Najua
ni kipa mzuri mwenye uwezo na uzoefu wa kutosha na kipindi hiki
najivunia kuwa na makipa watatu wenye uwezo mzuri. Yaliyopita
yameshapita, yalikuwa ni timu ya Taifa na sasa tumekutana Yanga. kazi
yetu ni moja tu kuifanya klabu iwe kwenye hadhi ya Kimataifa zaidi”.
Kauli
hii ilionesha ukomavu wa Maximo. Kipindi kile ilikuwa timu ya Taifa,
lakini sasa wanaungana Yanga kufanya kazi moja ya kuisaidia klabu.
Kwa maisha ya wengi ni ngumu kufanya kazi na mtu mliyekuwa naye na `bifu` na hii inatokana na kuendekeza chuki za ajabu.
Kama mlikuwa na `bifu` na mtu mkiwa Yanga, kwanini muendeleze `bifu` mkikutana Simba au Azam fc?
Kibongo
bongo inawezekana kwasababu wengi hawana nidhamu na kujali kazi. Maximo
anaamini Kaseja anaweza kumsaidia. Hawezi kukumbuka ya Taifa stars
akiwa Yanga.
Huu
ni mtazamo sahihi na naamini wanachama na mashabiki wa Yanga wanatakiwa
kumsapoti Maximo ili Kaseja arejee kwenye kiwango chake.
Bado ni kijana, ana miaka 29. Kaseja ana miaka mingi ya kucheza mbeleni, lazima aaminiwe.
Bahati
nzuri viongozi wa Yanga wametambua haraka na kumuacha aendelee
kuichezea timu hiyo msimu ujao. Naamini Kaseja atafanya kazi nzuri
akiaminiwa.
Mashabiki punguzeni presha juu yake, mnamharibia ufanisi wa kazi.
Kuwa
na makipa watatu wenye uzoefu, Juma Kaseja, Deo Munish `Dida` na Ally
Mustafa `Barthez` ni faida kwa klabu. Waacheni wachuane katika mazoezi
ya kocha wa makipa, Juma Pondamali `Mensah` na mwenye kiwango ataanza
chini ya Maximo.
0 comments: