|
Picha na Maktaba |
MBUNGE
wa Urambo Magharibi, Prof. Juma Kapuya (CCM), ambaye pia ni Waziri wa
Ulinzi wa zamani, jana alijikuta katika wakati mgumu wa kuumbuliwa na
mbunge mwenzake wa Temeke, Abbas Mtemvu (CCM), wakati wawili hao
wakibishania uuzwaji tata wa Kampuni ya Usafiri Dar es Salaam
(UDA).Hatua hiyo ilijitokeza wakati Mtemvu akichangia hotuba ya bajeti
ya Wizara ya Fedha na Uchumi kwa mwaka wa fedha 2014/2015, na kuungana
na wabunge wenzake kadhaa waliotangulia kuchangia, akidai UDA imeuzwa
kifisadi bila wabunge wa Mkoa wa Dar es Salaam kushirikishwa.
Wakati
Mtemvu akiendelea kujenga hoja yake, Prof. Kapuya aliomba kumpa
taarifa, akimweleza kuwa mbunge kujishughulisha na uwekezaji si dhambi
na kwamba UDA imeuzwa kihalali wala hakuna ufisadi kama inavyodaiwa,
isipokuwa mbunge huyo anatumika kuwashawishi wabunge kupinga suala hilo.
Baada ya Prof. Kapuya kuketi,
Mtemvu
aliendelea kuchangia akidai kuwa haipokei taarifa ya mbunge mwenzake
kwa sababu yeye ni miongoni mwa walioshirikia kuiuza UDA kifisadi
akitumia nafasi yake ya uwaziri.
“Yaani
mtu mzima unasimama hapa unasema kwamba UDA iliuzwa kihalali wakati
wewe ulitumia nafasi yako ya uwaziri kushiriki ufisadi huo?” Alihoji
Mtemvu na kuongeza kuwa yeye hatumiki bali Prof. Kapuya ndiye anazunguka
hotelini Dodoma kuwashawishi wabunge watetee uuzwaji wa UDA na kutamba
kuwa video kamera zipo zikimuonyesha akifanya hivyo.
Wakati
Mtemvu akieleza hivyo, wabunge wengi walimshangilia kwa nguvu, hususani
wale wa kutoka Mkoa wa Dar es Salaam, ingawa Naibu Spika, Job Ndugai,
aliingilia kati na kumtaka ajielekeze kwenye hoja badala ya kuendeleza
mashambulizi binafsi.
Mkulo afunguka
Waziri
wa Fedha na Uchumi wa zamani, Mustafa Mkulo amevunja ukimya na kutoa
siri ya uuzaji wa kiwanja cha Shirika Hodhi la Mali za Serikali (CHC).
Kiwanja hicho ambacho Mkulo alidaiwa kukiuza kifisadi ni kile kilichopo
Barabara ya Nyerere, jijini Dar es Salaam.
Akijibu
tuhuma hizo kwa mara ya kwanza, Mkulo alisema kiwanja hicho kimeuzwa
kama ilivyouzwa UDA ambayo hadi sasa ipo kwenye mzozo mkubwa unaoligawa
Bunge.
Alisema
yeye wala wizara yake, hawakuhusika na uuzwaji wa kiwanja hicho ambacho
kwa mara ya kwanza alitajwa bungeni kuwa mhusika mkuu na mwizi namba
moja. Akichangia hotuba ya bajeti ya Wizara ya Fedha na Uchumi kwa mwaka
wa fedha 2014/2015, Mkulo alisema waliohusika na uuzwaji wa kiwanja
hicho ni aliyekuwa Mwenyekiti wa Bodi ya CHC, Prof. Khamis Mahigi na
aliyekuwa Mkurugenzi wa shirika hilo, Methusela Mbanjo.
“Aprili
mwaka 2012, nilituhumiwa kuuza kiwanja hicho, leo nataka kutoa
ufafanuzi kwa sababu nimepata nafasi, mimi sikuuza wala sikushiriki
mchakato wa kuuza kiwanja. “Bodi ya CHC iliandikia Wizara ya Fedha barua
ya kuomba kibali cha kuuza kiwanja chao, barua hiyo haikwenda wizarani
isipokuwa ilikwenda kwa Msajili wa Hazina, ambaye baada ya uchambuzi wa
kina akatoa ushauri kwa Katibu Mkuu naye akatoa mapendekezo yake kwa
Waziri wa Fedha nini kifanyike.
“Mapendekezo
ya msajili yalionyesha udhaifu kwenye maombi ya CHC ambapo baada ya
kuona upungufu huo, nikiwa waziri nikaagiza bodi ifuate taratibu, kanuni
na sheria kisha ilete upya kwa sababu hiyo ni mali ya serikali. “Baada
ya siku chache wizara ikapata taarifa kwamba CHC ilikuwa imeshapokea
nusu ya gharama ya mauzo ya kiwanja kile, kwa maana kwamba bodi ilikuwa
imeshauza kiwanja na barua kwamba waziri atoe kibali ilikuwa ni
geresha,” alisema Mkulo ambaye ni mbunge wa Kilosa (CCM).
Mkulo
alisema kuthibitisha kwamba hakuhusika na uuzwaji wa kiwanja hicho,
mkataba wake ulisainiwa miezi mitano baada ya yeye kuondoka hazina.
Alisema karatasi na nyaraka zote zilizotumwa kwenye magazeti zilikuwa
feki, lakini zilitoka CHC.
Mkulo
alisema wabunge waliomlipua bungeni walikuwa wakipita na nyaraka hizo
huku wakimtuhumu kuwa yeye ni mwizi namba moja.“Kiwanja hiki kiliuzwa na
wenyewe kama ilivyouzwa UDA, ila hii ni mbaya zaidi ya UDA.
“Nikisema
niyaseme yote hapa wabunge wenzangu mtatapika, wakati ule yanatokea
bungeni mimi nilikuwa Washington DC kwenye mkutano wa Benki ya Dunia,
niliomba nafasi kutoa utetezi wangu humu bungeni, lakini kwa bahati
mbaya sikupata hadi nilipoondoka Hazina,” alisema.
Mkulo
alisema kuwa aliona ayaseme hayo jana kwani yeye ni Muislamu, marehemu
baba yake alikuwa sheikh na babu yake alikuwa chifu, na hivyo anataka
afe kwa heshima kwa kusema ukweli.
0 comments: