BAJETI KUU YA SERIKALI YA MWAKA 2014/2015 YAPITISHWA GIZANI BUNGENI DODOMA.
Wabunge wakisoma kwa kutumia mwanga wa tochi za simu ndani ya Bunge jana mara baada ya umeme kuzima katika ukumbi huo wakati walipokuwa wakipiga kura kupitisha Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2014/15. Picha na Edwin Mjwahuzi.
Bajeti Kuu ya Serikali ya 2014/15 imepitishwa jana bungeni mjini hapa na Waziri wa Fedha, Saada Mkuya akisema lazima wafanyabiashara walipe kodi inayostahili na iwapo kuna anayedhani anapata hasara kwa kulipa kodi afunge biashara.
Akihitimisha mjadala wa bajeti hiyo kabla ya umeme kukatika wakati wa upigaji kura kuipitisha, Mkuya alisema kama mfanyakazi anatozwa kodi, mfanyabiashara anayepata faida hataachwa.
“Mfano hata hapa Dodoma wanakuja kuzungumza na ninyi wabunge ili kuanza kuwafanyia ushawishi ili muwasaidie katika kukwepa kodi, hilo haliwezekani,” alisema.
Alikemea wizi wa fedha za umma unaofanywa na watumishi wa Serikali akisema unaumiza taifa na kuifanya Serikali ipate hasara kubwa.
“Mfano kuna wakati mtu mmoja alileta taarifa za kuidai Serikali Sh600 milioni, lakini tulipokwenda kuhakiki tukagundua kuwa alikuwa anadai Sh600,000 tu, sasa wabunge tunaposema kuna wizi, basi lazima muamini kuwa huo ndiyo wizi wa mali ya umma,” alisema Mkuya.
Alisema uhakiki huo ulipunguza deni la taifa kutoka Sh19 bilioni hadi Sh5 bilioni ambalo ndilo deni halisi kwa wadai wa ndani.
Mkuya alisema kuanzia sasa, Serikali haitalipa fedha zozote za deni hadi uhakiki ufanyike kwa kuwa wizi umezidi ikiwamo katika ununuzi wa magari na sasa hakutakuwa na taasisi itakayoruhusiwa kununua magari yake hadi kwa kibali maalumu cha Hazina na yote yatanunuliwa kwa pamoja kutoka kwa mzalishaji bila kupitia mawakala.
“Katika hilo tumejipanga pia kuhakikisha kuwa hatupeleki fedha katika taasisi zozote ambazo hazitaleta ripoti ya utekelezaji.”
Kuhusu suala la mikopo, alisema kuwa Tanzania itaendelea kukopa kwa ajili ya maendeleo kwa kuwa deni la taifa linahimilika kwa vyanzo vyake vyote, hivyo kusema wasikope siyo sahihi.
Akizungumzia suala la magari chakavu ambalo lilipigiwa kelele na wabunge wengi, alisema msimamo wa Serikali utabaki hivyo kwamba magari yanayoanzia umri wa miaka minane na kuzidi ni lazima yatozwe ushuru mkubwa.
Alisema wamefanya hivyo baada ya kubaini kuwa Tanzania imefanywa kuwa dampo la kutupa magari mabovu kutoka maeneo mbalimbali duniani.
Alisema baada ya kubaini kuwa magari yaliyozidi muda huo yamepandishwa kodi hapa nchini, bei za magari ya Toyota nchini Japan zimeshuka.MWANANCHI
0 comments: