SAMWEL SITTA ATUHUMIWA KUPENDELEA BAADHI YA WAJUMBE WA KATIBA



MJUMBE wa Bunge Maalumu la Katiba, Khamis Kigwangala, amemtuhumu Mwenyekiti wa bunge hilo, Samuel Sitta, kuliendesha kwa upendeleo, uonevu na ushabiki.
Kigwangala alisema Sitta, amekuwa na tabia ya kupendelea wachache huku akidai kufanya hivyo ni kutenda haki, jambo ambalo si sahihi.
Kigwangala alitoa tuhuma hizo jana asubuhi alipotaka mwongozo wa Mwenyekiti juu ya muda wa dakika 16 alizopewa Msemaji wa wachache, Tundu Lissu, kumalizia hotuba yake iliyokatishwa wiki iliyopita baada ya TBC kukatisha matangazo ya moja kwa moja.
Kigwangala alisema Lissu, alikuwa amebakiza dakika mbili, lakini alishangazwa na uamuzi wa Sitta kuwa mjumbe huyo amebakiza dakika 16.
“Mimi pia niliambiwa wakati nasoma hoja ya kamati yangu, lakini TBC walikuwa wakikata matangazo lakini nilipokuandikia kuhusu jambo hili hukunisikiliza, lakini kwa Lissu naona unafanya hivyo, sasa unaona kuwapendelea wachache ndiyo kutenda haki?” alihoji.
Akijibu mwongozo huo, Sitta alisema tuhuma hizo zimemsikitisha kwa kuwa mambo mengi anayoyafanya anategemea wataalamu waliopo bungeni hapo.
“Nasikitika kutuhumiwa nafanya upendeleo, mimi nategemea wataalamu wao ndiyo wanashika saa na wao ndiyo wanasema umebaki muda fulani, mimi sitazami saa yangu na kuamua.
“Ikiwa hawa watatu wamekosea basi ni bahati mbaya wao ndiyo wamesema hizo dakika 16 si mimi, ni kweli jana Jumapili, uliniletea barua nyumbani kulalamikia kuhusu kutopewa nafasi kama Lissu,” alisema.
Sitta alisema baada ya kuipata barua ya Kigwangala alimpa maelekezo Katibu wa Bunge afuatilie TBC, kujua kama lina ukweli ndani yake na baadae ilithibitika kuwa wakati wa Kigwangala akiwasilisha maoni hakukuwa na tatizo la kukatika kwa matangazo.
“Jamani hili la Lissu halikuwa langu, nilitahadharishwa na Mheshimiwa Freeman Mbowe, wote tukafuatilia tukabaini ni kweli,  sasa hili la Kigwangala, halikutolewa tahadhari,” alisema.

0 comments:

Copyright © 2013. MSANGIBIN ALLY - All Rights Reserved
Customized by: MSANGIYUSUPHALY | Powered by: KIINICHAHABARI
Designed by: http://kiinichahabaribongo1.blogspot.com/