MUNGU WANUSURU WALIOFIKWA NA ADHAA LA JANGA LA MUFURIKO:DAR SI SALAMA...ANGALIA MAPICHA


ALFAJIRI ya Alhamisi ya wiki iliyopita haitasahaulika kwa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam na viunga vyake ambapo maafa makubwa yalipoanza kufuatia mafuriko ya mvua zilizonyesha mfululizo na kusababisha vifo na uharibifu wa mali hivyo kuonesha wazi kuwa, kumbe Dar si salama.
Daraja linalounganisha wilaya ya Bagamoyo na Mkoa wa Dar es Salaam likiwa limekatika baada ya mvua kubwa kunyesha. Idadi ya vifo iliyoripotiwa mpaka juzi jioni ni kumi na mbili huku wanachi wengi wakikosa makazi na wengine kupotea kwa kusombwa na mafuriko.

UWAZI MZIGONI
Timu ya Uwazi ilizunguka sehemu tofauti za jiji zilizozizima na kushuhudia maafa hayo.
Tukio la kwanza ni kuonekana laivu kwa maiti ya mtu mmoja aliyezolewa na maji maeneo ya Jangwani wilayani Ilala.Mbali na kushuhudia uharibifu wa kutisha wa miundombinu na mateso ya watu walioathirika.
Helkopta ya Jeshi la Wananchi iliyokuwa imebeba viongozi wa serikali ikiwa imeanguka baada ya kupoteza mwelekeo. 
BARABARA ZAFUNGWA, MADARAJA YAZOLEWA
Uwazi lilishuhudia baadhi ya barabara zikiwa zimefungwa kufuatia kujaa maji na madaraja kuvunjika na mengine kuzolewa. Barabara zilizofungwa ni pamoja na Dar es Salaam – Pwani kwa daraja la Mto Mpiji kubomoka.
Pia Barabara ya Dar- Kibiti ilifungwa na kufanya magari ya kwenda Kusini kutofanya safari kwa siku ya Jumapili iliyopita.
Daraja la Mto Ruvu lilifungwa kutokana na maji kupita juu ya daraja hivyo kufanya usafiri wa kutoka Dar kwenda mikoani kuwa mgumu sanjari na kuingia jijini Dar.
MADARAJA YAFUNIKWA
Ndani ya Jiji la Dar madaraja mengi yalijaa maji ikiwa ni pamoja la Kinyerezi, Mlalakua, Mpiji Magoe kwenda Kidimu, Mbezi Mwisho, Msewe Kimara, Kijichi na Jangwani.
WAKAZI WAKOSA PA KUKAA
Baadhi ya maeneo ya jiji hasa Kigogo, Mwananyamala, Jangwani, Tandale, Mabibo na Tabata yalikumbwa na kadhia ya maji kujaa kwenye makazi ya watu na kusababisha wakazi wake kukaa kwenye mapaa kusubiri kuokolewa. WAZEE, WATOTO, WANAWAKE WAKATI MGUMU
Makundi yaliyoonekana kupata wakati mgumu kwa mafuriko hayo ni wazee, wanawake na watoto waliokuwa wakishindwa kupanda juu ya mapaa ya nyumba, hivyo kusimama kwa kubebana kwenye maji kwa muda mrefu, waliopata bahati waliokolewa na watu wenye nguvu wakiwemo vijana.
MAITI, MAJERUHI WAKIMBIZWA HOSPITALI
Uwazi lilishuhudia miili ikipelekwa Hospitali ya Taifa Mubimbili kwa hifadhi huku ikiwa na dalili ya kuharibika.
Idadi kubwa ya majeruhi ambao hali zao zilikuwa mbaya walikimbizwa katika Hospitali za Amana, Mwananyamala na Temeke.
MAENEO HATARI ZAIDI
Maeneo mengi jijini yameathirika, lakini ambayo hayako salama kabisa ni mabondeni kama Jangwani, Kigogo Sambusa, Tabata ya Matumbi, Mikocheni na Msasani.
KOVA, MKUU WA MKOA WAPATA AJALI
Jumapili asubuhi, Kamanda wa Polisi, Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova akiwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Mecky Sadik walipata ajali ya chopa kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere ‘JNIA’ walipokuwa wakijiandaa kwenda kutembelea sehemu zenye mafuriko.
DAR SI SALAMA
Imebainika kuwa, miundombinu ya maji jijini Dar ndiyo sababu ya kutokea kwa mafuriko makubwa kwa vile maji hukosa njia ya kupita na kutengeneza visiwa vidogovidogo kila mahali.
“Kama mnavyoona Dar si salama, iko siku jiji lote litafunikwa na maji. Mvua kidogo mafuriko, watu wanakufa. Yaani vifovifo njenje,” alisema mkazi mmoja wa Mwananyamala Kisiwani baada ya kunusurika na mafuriko.
WATAALAM WANENA
Wataalam mbalimbali wa masuala ya mabadiliko ya tabianchi wamebainisha kasoro kubwa katika mipango miji nchini kwamba haizingatii madhara yatokanayo na mabadiliko ya hali ya hewa na kuruhusu ujenzi holela mabondeni, milimani na kwenye mikondo ya maji, ikiwemo mifereji.
“Hatua ya kuruhusu makazi kwenye maeneo ya mabondeni na kwenye mapito ya maji huzuia mikondo ya maji hivyo mvua zinaponyesha maji yake hulazimisha njia na matokeo yake ni mafuriko yenye madhara makubwa kwa maisha ya watu na mali zao,” alisema mtaalam mmoja kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania ‘TMA’ huku akiomba hifadhi ya jina lake.
SERIKALI KUENDELEA KUGHARAMIA MADARAJA
Kwa mujibu wa mtaalam huyo, ujenzi wa barabara na madaraja nchini pia hauzingatii suala la mabadiliko ya tabianchi ambalo ni ajenda kuu kwa sasa duniani na ndiyo maana mvua nyingi Tanzania hubomoa madaraja na barabara na kuigharimu serikali mabilioni ya fedha kwa ajili ya ukarabati.

0 comments:

Copyright © 2013. MSANGIBIN ALLY - All Rights Reserved
Customized by: MSANGIYUSUPHALY | Powered by: KIINICHAHABARI
Designed by: http://kiinichahabaribongo1.blogspot.com/