ZISOME HAPA KAULI KUMI(10) ZILIZOVUTA HISIA ZA WENGI KWENYE BUNGE LA KATIBA MJINI DODOMA

Ni vigumu kueleza matukio yote yaliyotawala kauli na hisia za wengi kwa wiki nzima mjini Dodoma bila kuangalia  michango ya baadhi ya wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba.
Michango hiyo ya mawazo katika mjadala kuhusu rasimu ya kanuni zinazopaswa kuongoza kikao kwa siku 70 za kikao hicho, baadhi yake zilikuwa kali. 
Zifuatazo ni baadhi ya kauli hizo:

 1. Mchungaji Christopher Mtikila


Mtikila, ambaye ni mwenyekiti wa Democratic Party (DP), alitumia dakika tano kutoa somo kwa wajumbe wa Bunge hilo kuhusu umuhimu wa kupiga kura ya siri badala ya ile ya wazi.
Anasema haki ya kupiga kura kwa siri haitofautiani na haki ya mtu kuwa na miguu miwili na kwamba itashangaza akitokea mtawala akaamuru kila mtu awe na mguu mmoja, halafu watu wakakaa kujadili.
“Wote tutaonekana tuna matatizo ya akili,” alisema Mch. Mtikila.
Alisema Bunge Maalumu la Katiba litaingia katika hatia na aibu kwa kujadili mambo ya msingi ya kidemokrasia ambayo pia yameainishwa katika katiba ya sasa, likiwamo suala hilo la kura ya siri.
“Mwenyekiti (akimlenga Pandu Ameir Kificho) tumekuchagua kwa kura ya siri siyo kwamba tulikuwa wajinga kuliko wenzetu, hapana! Ni ‘democratic civility’ (ustaarabu wa kidemokrasia),” alisema.
 “Ni aibu waheshimiwa na hii nasema si jambo la mjadala kuna vitu vya kujadili, lakini si haki ya kupiga kura kwa siri. Hii ni haki ya msingi ya kidemokrasia,” alisema.

 2. Profesa Ibrahim Lipumba (Mwenyekiti –CUF Taifa)
Mwenyekiti huyo wa CUF alisema msingi wa kupiga kura ya siri ni kujaribu kuwalinda wajumbe ambao wanaweza kupiga kura kinyume na misimamo ya vyama vyao au makundi yao.
 Akijenga msingi wa hoja yake, Profesa Lipumba alisema hata Jaji Joseph Warioba katika taarifa yake alisema moja ya taasisi zilizotoa maoni ni Baraza la Wawakilishi lililopendekeza Serikali tatu.
“Tunadai kura za siri kusudi kuwalinda hawa wenzetu ambao wametoa misimamo, wakija kupiga kura hapa  inaweza kuwapa matatizo huko walikotoka,” alisema.
 Aliongeza : “Tunapolishabikia hili kuwa pasiwe na kura ya siri inaonekana wazi pana ajenda ya kuwashughulikia watakaokwenda kinyume cha msimamo.”





 3. Esther Bulaya (Viti Maalumu-CCM)
Bulaya, tofuti na wajumbe wenzake wengi kutoka chama tawala (CCM), alionekana kutoa mchango uliogusa hisia za wengi hasa pale alipoeleza bayana kuwa hayuko tayari kuona ukandamizaji unafanyika kumlazimisha apige kura ya wazi.
Akirejea msimamo wa kura ya wazi unaoshabikiwa na wajumbe wengi wanaotokana na chama chake, alisema hawezi kupiga kura ya aina hiyo wakati anajua inamnyima uhuru wake.
“Nitasema kweli daima, fitina kwangu mwiko. Ni lini na wapi katika uamuzi mgumu kama huu kulifanyika kura za wazi kama wengi wanavyotaka,” alisema.

  4. Pandu Ameir Kificho (Mwenyekiti wa Muda)

Naye Kificho, ambaye pia ni Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, alionyesha kukerwa na baadhi ya vyombo vya habari hasa vilipolishikia bango suala la posho.
 “Kusema kweli, jamii tunaichanganya mpaka  jambo hili la kutupatia Katiba Mpya lionekane ni la mchezo au tumekuja kudai posho. Nawataka wenzetu (wanahabari) wawe makini sana juu ya jambo hili wasiupotoshe umma ili kazi hii isiingie dosari,” alisema.
Vyombo vyote vya habari vizingatie kupata habari kwa uwazi na ukweli kutoka kwa wanaohusika ili jamii yetu ya Watanzania ipate habari za kweli na hilo la kupokea tu posho kwa kusoma magazeti tunalikanusha kwa nguvu zote”.

 5. Philemon Ndesamburo (Moshi Mjini-Chadema)
Ndesamburo aliwataka wajumbe wenzake kuacha ushabiki wa kisiasa na kutambua wanatengeneza katiba itakayodumu miaka 50 ama miaka 10 ijayo.
“Tusilete ushabiki. Nawaombeni sana tusilete ushabiki katika jambo hili. Hili ni jambo zito. Hili ni jambo tunalolifanya kwa niaba ya Watanzania milioni 45 na sisi tumepata bahati tu; ni Mungu ametusaidia,” alisema.

 6. Profesa Jumanne Maghembe (Waziri wa Maji)
Profesa Maghembe alifananisha upigaji wa kura kwa siri  kuwa sawa na ule uliofanyika nchini Marekani wakati wa kashfa ya ufuska iliyokuwa ikimkabili aliyekuwa rais wakati huo, Bill Clinton.
“Kule Marekani walikuwa wakipiga kura ya kumwondoa madarakani Clinton kwa madai ya kushikwa ugoni. Walipiga kura ya wazi kwa sababu lilikuwa jambo kubwa la kumwondoa mtu madarakani,” alisema.
 Profesa Maghembe, ambaye pia ni Waziri wa Maji, aliwasihi wajumbe kutofautisha upigaji kura wa mwenyekiti wa kijiji, diwani, mbunge na rais ambao alisema wananchi hupiga kura za siri.
“Humu ndani tunatafuta sheria mama ya nchi. Tumepewa jukumu hilo kwa niaba ya Watanzania wote. Wao watapata nafasi ya kusema ndiyo au hapana. Sasa tunajificha ili iweje, tunamficha nani?” alihoji.
7. Sheikh Hemed Jengo
Sheikh Jongo alishauri Bunge Maalumu la Katiba kuwapa nafasi wajumbe wanawake watakaokuwa katika hedhi, waruhusiwe kuapa bila kushika kitabu kitukufu, Quran.
“Siku nyingine kinamama wanakuwa katika siku maalumu (hedhi). Ni haramu kwa mujibu wa dini kushika msahafu. Atakapojieleza kuwa hali yangu si nzuri, basi aruhusiwe kuapa hivyo hivyo kwa heshima,” alisema na kuongeza:
“Hata kwa wanaume wa Kiislaamu wakitaka kuapa wachukue udhu kwa sababu kitabu chenyewe kinakataza kukishika bila ya udhu. Ndiyo yamini. Ndiyo maana watu wengine hatuoni wanafanya vizuri kule nje kwa sababu wanajua waliapa bila udhu na haikuwa yamini.”

 8. Maria Sarungi Tshehai
Mwanaharakati huyo alitumia fursa aliyopewa kuwaponda wajumbe wenzake waliokwenda katika Bunge hilo kwa ajili ya kuwasilisha masilahi ya vyama.
“Hatuko hapa kwa ajili ya kuwasilisha vikundi mbalimbali. Tukianza hivyo itakuwa ni hatari sana katika Bunge hili,” alisema.
“Nianze kwamba kitu kilichonifanya nitoke nje nilifutwa (na mtu ambaye hakumtaja jina). Aliniambia wewe mbona unaonekana upo kwenye upande wa chama fulani.” 

9.Richard Ndassa (Mbunge wa Sumve)
Yeye alionekana kukerwa na baadhi ya taarifa za vyombo vya habari kuhusu suala la posho na kuvishtaki vyombo hivyo kwa mwenyekiti wa muda wa Bunge hilo, Pandu Ameir Kificho.
 “Wabunge wanachota milioni 129 kwa kikao cha dakika 30” na kingine kikisomeka, “Wabunge walipwa milioni 130 kwa dakika 25; Bunge la Katiba vipande vipande; wapewa posho kwa kusoma magazeti,” alisema akikariri vichwa vya habari vya baadhi ya magazeti na kudai vinamkera.

10. Dk. Zainab Gama
Naye mwanasiasa mkongwe, Dk. Zainabu Gama alikwenda mbali na kudai kuwa baadhi ya wanaotaka kura ya siri wametumwa na watu ama wamekula rushwa ndiyo maana hawataki kupiga kura ya wazi.
“Hatukuletwa hapa kimchezo mchezo.  Simama, sema mimi uamuzi  wangu huu kila mmoja akuone,” alisema.

MWANANCHI

0 comments:

Copyright © 2013. MSANGIBIN ALLY - All Rights Reserved
Customized by: MSANGIYUSUPHALY | Powered by: KIINICHAHABARI
Designed by: http://kiinichahabaribongo1.blogspot.com/