UTAFITI :ULEVI WA SHISHA WASHIKA KASI BONGO..WAGUNDULIKA UNA MADHARA MAKUBWA



Umeibuka ulevi mpya nchini ambao umethibitika kuwateka vijana hasa wa jiji la Dar es Salaam, huku kukiwa na taarifa za kitaalamu kwamba ulevi huo una athari za kiafya kwa watumiaji.
Ulevi huo ni kupitia starehe au anasa mpya ya uvutaji shisha; ulevi ambao watengenezaji hutumia chombo maalumu chenye bomba la kutolea moshi, ambacho huwekwa tumbaku, maji na moto.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini kuwa tumbaku huwekwa katika chombo hicho na kuunguzwa kwa moto, kisha moshi wa tumbaku hupita kwenye maji na huingia kwenye bomba, kisha watumiaji huanza kuvuta.
Sehemu maarufu ambako shisha inauzwa ni Ufukwe wa Coco, maeneo ya Kinondoni, Mwananyamala, Sinza Barabara ya Shekilango na maeneo kadhaa ya mitaa ya mjini.
Mmoja wa watumiaji wa shisha, Ismail Ndunguru alisema yeye na vijana wenzake hutumia siku za mwisho wa wiki kwenda kuburudika kwa uvutaji katika hoteli moja iliyopo mjini, Mtaa wa Garden jijini Dar es Salaam.
“Kuvuta shisha kwa siku nzima ni Shilingi 10,000, mkimaliza, mnarudisha bomba. Tukiwa vijana wengi inafurahisha sana kuvuta,” alisema Ndunguru.
Taarifa za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaeleza kuwa, mkupuo mmoja wa shisha, una kemikali hai 4,800 na kwamba kemikali hizo husababisha saratani ya mapafu, maradhi ya moyo na maradhi ya mfumo wa upumuaji.
WHO inaeleza kuwa, kiasi cha uvutaji wa shisha kwa saa moja ni sawa na kuvuta sigara 100 au 200.
Daktari Bingwa wa magonjwa ya ndani ya mwili na mfumo wa hewa, Meshack Shimwela alisema madhara ya shisha ni kama yale yanayosababishwa na uvutaji wa sigara pengine na zaidi kutokana na kilevi hicho kuwa na tumbaku nyingi.
Dk Shimwela alisema licha ya kuwa watengenezaji na wavutaji wa shisha hudai kuwa haina madhara kwa sababu huchanganywa na maji, lakini bado madhara yake ni makubwa.
“Marahi yote yanayosababishwa na uvutaji wa sigara ndiyo yanayosababishwa na shisha, kwa mfano saratani ya mapafu na mdomo, kifua kikuu na mzio ambao unaweza kusababisha pumu,” alisema Dk. Shimwela.
Dk. Shimwela alisema ni vizuri watumiaji wakajua madhara ya shisha, badala ya kuchukulia kuwa ni mtindo wa maisha tu au starehe isiyo na madhara.

0 comments:

Copyright © 2013. MSANGIBIN ALLY - All Rights Reserved
Customized by: MSANGIYUSUPHALY | Powered by: KIINICHAHABARI
Designed by: http://kiinichahabaribongo1.blogspot.com/