TAARIFA TOKA KURUGENZI YA MAWASILIANO IKULU
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete
asubuhi ya kesho, Ijumaa, Machi 14, atamwapisha Katibu wa Baraza la
Wawakilishi Bwana Yahya Khamis Hamad kuwa Katibu wa Bunge Maalum la
Katiba.
Aidha, katika sherehe fupi itakayofanyika
Ikulu Ndogo, Dodoma, Rais Kikwete atamwapisha Katibu wa Bunge la
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Thomas Didimu Kashililah kuwa
Naibu Katibu wa Bunge Maalum la Katiba.
Taarifa iliyotolewa jioni ya leo,
Alhamisi, Machi 13, mwaka huu wa 2014 mjini Dodoma na Katibu Mkuu
Kiongozi, Balozi Ombeni Y. Sefue inasema kuwa Rais Kikwete atawaapisha
Katibu na Naibu Katibu wa Bunge Maalum la Katiba kwa mujibu wa kifungu
cha 24(7) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83, toleo la mwaka
2014.
Bwana Hamad na Dkt. Kashilillah wanashika
nafasi hizo kwa mujibu wa Kifungu cha 24(1) cha Sheria ya Mabadiliko ya
Katiba, Sura ya 83, toleo la mwaka 2014, ambacho kinasema kuwa nafasi
za Katibu na Naibu katibu wa Bunge Maalum la Katiba zitajazwa na Katibu
wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Katibu wa Baraza la
Wawakilishi, Zanzibar.
Kwa mujibu wa kifungu cha 24(3) cha
sheria hiyo, Sura ya 83, toleo la mwaka 2014, Katibu wa Bunge Maalum
atatoka upande tofauti na ule anakotoka Mwenyekiti wa Bunge Maalum.
Kwa vile aliyechaguliwa kuwa Mwenyekiti
wa Bunge Maalum, Mheshimiwa Samuel John Sita anatoka Tanzania Bara, basi
Katibu wa Bunge anakuwa Bwana Yahya Khamis Hamad ambaye ni Katibu wa
Baraza la Wawakilishi, Zanzibar na Naibu Katibu wa Bunge Maalum la
Katiba anakuwa Dkt. Kashililah ambaye ni Katibu wa Bunge la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania.
Mwisho.
Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
13 Machi,2013
0 comments: