MATESO! MIAKA 14, KILO 111, ASIMAMISHWA SHULE...TAZAMA MAPICHA HAPA



GRACE Simon mwenye miaka 14 anateseka na uzito wa kupindukia wa kilo 111 (kama gunia moja la mahindi na viroba vitatu) hali iliyomsababishia akatishwe masomo na walimu katika Shule ya Msingi Amani, Ukonga, Ilala jijini Dar es Salaam alikokuwa anasoma.

Grace Simon mwenye miaka 14 anateseka na uzito.
Grace ambaye mwaka huu angekuwa darasa la saba lakini aliachishwa shule mwaka 2010 akiwa darasa la nne na walimu wakimtaka akatibiwe.

MAMA MZAZI ASIMULIA

Akizungumza na Uwazi kuhusu mkasa mzima wa mtoto Grace, mama yake mzazi, Ashura Bakari alisema binti yake alimzaa salama mwaka 2000 lakini ilipofikia mwaka 2002 akiwa na miaka miwili alianza kuvimba tumbo hali ambayo hakujua chanzo chake.


ATENGWA NA WANAFUNZI
Mama huyo akizungumza kwa masikitiko alisema kuwa, Grace alipofika darasa la nne, akiwa na umri wa miaka kumi baadhi ya wanafunzi wenzake walianza kumnyanyapaa kutokana na unene ambao ulikuwa ukiongezeka siku hadi siku.

“Walikuwa wakimtania sana mwanangu hadi kukosa amani. Hali hiyo iliwafanya walimu kumsimamisha masomo ili atibiwe. Hadi sasa sijapata msaada wa kupona kwake,” alisema mama huyo huku machozi yakimtoka.

HOSPITALI ZIMESHINDWA?
Aidha, mama Grace aliongeza kuwa amekwishahangaika katika hospitali mbalimbali za jijini Dar es Salaam, ikiwemo Muhimbili bila mafanikio.

“Muhimbili waliniambia ili mwanangu aweze kufanyiwa vipimo pamoja na matibabu gharama zake ni shilingi laki nane (800,000) ambazo nimezikosa na hakuna mtu wa kunisaidia,” alisema.

NDUGU NAO

Alisema mbali na kutafuta tiba hospitalini, amekuwa akipita huku na huko kuomba msaada wa fedha kutoka kwa ndugu na jamaa lakini hakuna aliyemsadia.

KWA NINI BABA MZAZI ASIMSAIDIE?

Katika hali ya kushangaza, mama huyo alisema ili kupata fedha hizo anahangaika peke yake kwa sababu baba mzazi wa Grace, Simon alikataa kutoa msaada wowote.

“Baba yake yupo hai, alikuwa anatoa msaada kipindi cha mwanzo lakini miaka kama mitano imepita hakuna msaada anaonipa. Ni kweli hatuishi pamoja lakini mtoto tulizaa wote,” alisema kwa masikitiko makubwa mama huyo.

WALICHOKIONA MADAKTARI

Akizungumzia kiini cha tatizo, mama huyo alisema: “Kwa mujibu wa madaktari mwanangu anasumbuliwa na moyo kujaa mafuta mengi, kwa hiyo homoni zake zimekosa uwiano na ini pia lina sumu nyingi.”

GRACE AWALILIA WATANZANIA
Akizungumza na mwandishi wetu, mtoto huyo anayetamani kuendelea kusoma aliwaomba Watanzania wamsaidie fedha ili aweze kutibiwa na kurejea darasani.

“Niliachishwa shule ili nitibiwe, nikipona nirejee shuleni, lakini hadi sasa sijapata nafuu, na ninajua ni kutokana na kutopata matibabu sahihi,” alisema Grace huku akilia.

UONGOZI WA SHULE

Mmoja wa walimu waandamizi wa Shule ya Msingi Amani alipokuwa akisoma mwanafunzi huyo (hakuwa tayari kutaja jina lake), alikiri kumtambua mwanafunzi huyo na kusema aliachishwa shule kwa hofu ya uongozi wa shule.

“Hatukumwachisha shule kwa nia mbaya, lakini lengo letu lilikuwa akatibiwe kisha arudi shuleni lakini matibabu anayopata hajaweza kupona na hali aliyokuwa nayo inazidi kuongezeka siku hadi siku,” alisema mwalimu huyo.

Akaongeza: “Mwaka huu Grace ilikuwa awe darasa la saba, lakini hata kutembea ni tatizo hali ambayo tuliona kuwa unene ule si afya bali ni ugonjwa.”

MSAADA UNAAOHITAJIKA

Kwa yeyote aliyeguswa na tatizo la Grace ambaye anasaka shilingi laki nane tu ili atibiwe, anaweza kuwasiliana na mama yake mzazi kwa simu: 0719 465445, ASHURA BAKARI.

credit: GPL

0 comments:

Copyright © 2013. MSANGIBIN ALLY - All Rights Reserved
Customized by: MSANGIYUSUPHALY | Powered by: KIINICHAHABARI
Designed by: http://kiinichahabaribongo1.blogspot.com/