JE WAJUA KUWA SERIKALI YANUNUA BUNDUKI 500 ZA AK47 KUKABILI UJANGILI
Silaha
hizo zimepatikana ikiwa ni takriban wiki mbili tangu Rais Jakaya
Kikwete abanwe na vyombo vya habari vya kimataifa akitakiwa kueleza
mikakati iliyopo kupambana na ujangili ambao umeharibu sura ya Tanzania
nje ya nchi.PICHA|MAKTABA
Siku
moja baada ya Tanzania kutajwa na Shirika la Polisi la Kimataifa
(Interpol) kuwa kinara wa biashara ya meno ya tembo Afrika Mashariki,
Serikali imelipia kodi na kukabidhiwa bunduki 500 aina ya AK47 ili
kukabiliana na ujangili katika hifadhi na mapori ya akiba nchini.
Waziri
wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu alisema jana kuwa silaha hizo
zilizokuwa chini ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), tangu Novemba 2012
kutokana na kutokulipiwa kodi, zitasambazwa Ngorongoro, Selous, pamoja
na Hifadhi za Taifa za Tanapa.
Kati ya silaha hizo, 250 zitapelekwa Idara ya Wanyamapori, 200 Tanapa na 50 Mamlaka ya Hifadhi Ngorongoro.
Alisema
silaha hizo zimekombolewa ikiwa sehemu ya kutekeleza maazimio ya Bunge
na ahadi ya Serikali kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maliasili, Ardhi
na Mazingira.
Akizungumzia
sababu za kuchelewa TRA, Nyalandu alisema kulikuwa na ubishi wa ama
zilipaswa kulipiwa kodi au la, lakini mamlaka hiyo ilifafanua kuwa hayo
ndiyo matakwa ya sheria, hivyo akaamua kutoa fedha hizo.
Alipoulizwa
ni jinsi gani Serikali itadhibiti silaha hizo, Nyalandu alisema wizara
yake inaandaa miiko ya matumizi yake ikiwamo kufuatilia makabidhiano
yake na askari wanaokabidhiwa.
“Kumbuka
hizi si silaha za kwanza kuwa nazo, tunazo nyingine za AK47 na hizo
zimetuwezesha kukamata silaha haramu zaidi ya 2,000 zinazotumiwa na
majangili,” alisema.
Silaha
hizo zimepatikana ikiwa ni takriban wiki mbili tangu Rais Jakaya
Kikwete abanwe na vyombo vya habari vya kimataifa akitakiwa kueleza
mikakati iliyopo kupambana na ujangili ambao umeharibu sura ya Tanzania
nje ya nchi.
Itakumbukwa
kuwa miezi miwili iliyopita, Rais Jakaya Kikwete alilazimika kupangua
Baraza la Mawaziri na kuwatimua mawaziri wanne kutokana na vitendo vya
kinyama vilivyobainishwa na Kamati ya Bunge ya Maliasili na Mazingira
wakati wa Operesheni Tokomeza Ujangili.
Majangili papa 40
Akijibu
maswali ya waandishi wa habari, Waziri Nyalandu alisema majina ya
majangili papa 40 ambayo Rais Kikwete alisema anayo, ‘yatabandikwa’ hivi
karibuni.
“Serikali
ina mkono mrefu sana, hatupendi mtu aache mke na watoto wake afungwe
miaka 50. Kama ni majina tutayabandika, nimeshakubali, tutayabandika, ni
kwamba tu sina hiyo orodha hapa,” alisema.
Alisema, Serikali inawafahamu majangili hao kwa undani, wanapokunywa chai, wanapotembelea na shughuli zao za kila siku.
Alisema
majina yao si siri kwani tayari wameshafunguliwa mashtaka na wapo chini
ya mfumo wa Mahakama na wamekamatwa na vidhibiti.
Hivi
karibuni, Rais Kikwete alihojiwa na Shirika la Utangazaji la Uingereza
(BBC), alisema Serikali ina majina 40 ya majangili papa na mkuu wao yuko
Arusha.
Selous Yaimarishwa
Katika
hatua nyingine, Nyalandu alitangaza kuzipandisha hadhi kanda nane
zilizopo katika Pori la Akiba la Selous ili ziweze kujitegemea
kiutendaji kwa kuweka mkuu wa kila kanda.
Alisema
pori hilo lina ukubwa unaokaribia hifadhi zote za Taifa chini ya
Tanapa, jambo linalolifanya kuwa kubwa kimenejimenti na kiuendeshaji.
Pori la Selous lina kilomita za mraba 55,000 wakati mapori yote nchini kwa ukubwa wake ni kilomita za mraba 57,000.
Katika
kuweka mazingira ya uangalizi wa kina ya kupambana na ujangili
aliiagiza Idara ya Wanyamapori kukamilisha mchakato wa kufungua akaunti
maalumu za benki kwa kila kanda ili kuwawezesha wakuu wa kanda
kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
MWANANCHI
0 comments: