CHADEMA WAMPITISHA RASMI MGOMBEA UBUNGE CHALINZE

Mgombea
Ubunge wa Chalinze kwa tiketi ya Chadema, Mathayo Torongey akizungumza
na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana baada ya kutambulishwa.
Dar es
Salaam. Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema),
kimempitisha Mathayo Torongey kuwa mgombea rasmi wa ubunge kwa tiketi ya
chama hicho katika uchaguzi mdogo wa Jimbo la Chalinze.
Akimtambulisha
mgombea huyo kwa Waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana,
Mkurugenzi wa Bunge na Halmashauri wa Chadema, John Mrema alisema
Torongey alipitishwa juzi na Sekretariati ya chama kwa niaba ya kamati
kuu.
"Kikao cha
Sekretariati kilizingatia maoni na ushauri wa wanachama na viongozi wetu
wa ngazi za chini, Hivyo kwa kuwa hakukuwa na kipingamizi chochote juu
ya agombea, chama kilimpitisha Torongey" alisema Mrema.
Torongey
alishinda kura za maoni za chama hicho jimboni Chalinze kwa kupata kura
280 dhidi ya 510 zilizopigwa. Aliwashinda wapinzani wake, Omar Mvambo
aliyepata kura 84, Francis Mgasa 61 na Frank Mzoo alijinyakulia kura 23.
Mgombea
huyo anatarajia kushindana na Fabian Leonard aliyepitishwa na chama cha
CUF pamoja na Ridhiwani Kikwete anayesubiriwa kupitishwa na kamati kuu
ya CCM (CC-CCM).
Mshindi
wa uchaguzi huo anatarajia kuziba pengo la aliyekuwa mbunge wa jimbo
hilo, Said Bwanamdogo aliyefariki Januari 22 mwaka huu.
Mrema
ambaye pia ameteuliwa kuwa Mkuu wa Operesheni wa Uchaguzi mdogo wa
Chalinze, alisema Chadema kina imani kubwa na Torongey kushinda uchaguzi
wa jimbo hilo unaotarajia kufanyika Aprili 6.
Alisema
uchaguzi wa jimbo hilo ni muhimu sana kwa chama kwa kuwa limeshawahi
kuongozwa na Rais Jakaya Kikwete kwa miaka 15 bila ya kuwa na maendeleo
yoyote.
Mrema
alisema Chadema hakitishwi na historia ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya
kuwapitisha baadhi ya watoto wa vigogo katika chaguzi ndogo mbalimbali
za ubunge zilizowahi kufanyika nchini kama njia ya kuwarithi wazazi wao.
Alizitaja
chaguzi zile za Arumeru Mashariki ambapo CCM kilimpitisha Sioi Sumari
kumrithi baba yake marehemu Jeremia Sumari, Kalenga; Godfery Mgimwa
kumrithi William Mgimwa, na hatimaye uchaguzi wa Chalinze ambapo mtoto
wa Rais Kikwete, Ridhiwani anatarajia kuwania.
Naye
aliyekuwa mgombea katika kura za maoni katika kinyang'anyiro cha ubunge
ndani ya chama hicho, Omari Mvambo alisema aliridhishwa na matokeo na
mchakato mzima wa uchaguzi.
"Mchakato
mzima wa uchaguzi ulienda vizuri na wagombea wote tuliridhika na
matokeo yalikuwa sahihi. Kwa hiyo nimeamua kujidhihirisha kuwa ntampa
nguvu mgombea aliyepitishwa kushinda uchaguzi," alibainisha Mvambo.
Mgombea
aliyepitishwa na Chadema, Torongey alisema kuwa anatarajia sifa yake ya
uenyeji na historia ya maisha yake duni vitakuwa moja ya chachu za
kushinda wapinzani wake katika uchaguzi unaotarajiwa kuwa na upinzani
mkubwa.
Alisema
akipata ridhaa ya kuwa mbunge wa jimbo hilo, atahakikisha anatatua
changamoto za maji, elimu na pia kushughulikia masuala ya mgogoro baina
ya wafugaji na wakulima uliodumu kwa muda mrefu.Mgombea huyo alichukua
fomu maalumu ya tume ya uchaguzi Mjini Bagamoyo jana ya kugombea ubunge
wa jimbo hilo la Chalinze.
Chanzo, mwananchi
0 comments: