MJADALA WA MAPEPENDEKEZO YA RASIMU YA KANUNI YA UENDESHAJI BUNGE MAALUM LA KATIBA LAWATESA WABUNGE MJINI DODOMA.

“Nimeambiwa Siwa itakayotumika tayari imeshatengenezwa, nafikiri kesho inaweza kuletwa wajumbe mkaiona.”Ameir Pandu Kifich


DODOMA. 

SUALA la kura za siri au za wazi limeendelea kuwagawa wabunge ambao jana walivutana kufikia uamuzi wa aina ya kura zinazofaa kupigwa kupitisha Rasimu ya Katiba.
Malumbano hayo yaliibuka jioni ndani ya ukumbi wa Bunge wakati wajumbe walipokuwa wakijadili mapendekezo ya Rasimu ya Kanuni ya Uendeshaji Bunge Maalumu la Katiba.


Katika mjadala huo, wajumbe ambao wanatoka kundi la Chama Cha Mapinduzi ndiyo waliokuwa wa kwanza kutoa hoja zao huku wakishangiliwa na wenzao kabla ya kibano kuwageukia.


Wajumbe Henry Shekifu, William Lukuvi, Mohammed Aboud Mohammed, Pindi Chana na Profesa Anna Tibaijuka walitaka hoja ya kupiga kura kwa siri iondolewe na watu wapige kura za wazi.


Hoja hiyo ilipingwa na baadhi ya wajumbe, akiwamo Ester Matiku na Hija Hassan Hija na kufanya baadhi ya wajumbe wa bunge hilo kuwashangilia kwa mtindo wa kugonga meza.


Profesa Tibaijuka alieleza uzoefu wake kuwa kupiga kura kwa siri hakutaleta maana na kwamba, hata mataifa makubwa kama Marekani hupiga kura za wazi kutoa uamuzi.


Wajumbe wengine waliounga mkono hoja ya kura za siri ni Salmin Awadh Salmini na Paul Makonda, ambao nao walisema suala la usiri katika kura halitakuwa na maana kwani Watanzania wanataka kusikia misimamo ya wajumbe wao ambao wamewatuma.


Hata hivyo, kibao kiligeuka na ukumbi mzima kulipuka kwa shangwe baada ya wajumbe wengine kutaka kura ziwe za siri huku wakitoa mifano mbalimbali na faida ya kupiga kura za siri.


Wajumbe hao ni Mchungaji Ernest Kadiva na Ester Matiko ambao kwa nyakati tofauti walipendekeza kura za siri wakiunga mkono mapendekezo ya Kamati ndogo ya Kanuni iliyoongozwa na Profesa Costa Mahalu.


Mchungaji Kadiva alitahadharisha kuwa wapo watu ambao wameingia humo kwa misimamo ya vyama vyao, hivyo kupiga kura kwa uwazi itawapa shida kutoka waumini wa vyama hivyo.


Naye Matiko alisema kura ya siri ndiyo pekee ambayo inaweza kutoa haki kwa wajumbe kutenda haki na kwa uhuru.


“Kura zote lazima ziwe kwa siri maana hata wewe mwenyekiti wetu tulikuchagua kwa kura za siri, lakini Rais, wabunge na madiwani tunawachagua kwa siri leo mnakwepa nini kupiga kura za siri?” Alihoji Matiko. MWANANCHI

0 comments:

Copyright © 2013. MSANGIBIN ALLY - All Rights Reserved
Customized by: MSANGIYUSUPHALY | Powered by: KIINICHAHABARI
Designed by: http://kiinichahabaribongo1.blogspot.com/