UNDANI VIFO VYA WATOTO 3 NDANI YA BWAWA INASIKITISHA!
Mmoja kati ya marehemu aliyepatwa na janga hilo.
KUFUATIA vifo
vya watoto watatu waliokufa kwa pamoja ndani ya bwawa la kuogelea
‘swimming pool’ kwenye Hoteli ya Landmark, Mbezi Beach jijini Dar,
undani wa vifo hivyo umejulikana, Amani lina kisa kamili.
CHANZO
Kwa
mujibu wa chanzo chetu, watoto walionusurika kufa ambao walikuwa
wakisherehekea siku ya kuzaliwa ya mwenzao ‘bethidei’ aliyejulikana kwa
jina la Derrick Mboka, waliwaona marehemu wakielea kwenye maji ya bwawa
hilo walilosema kuwa ni la kuogelea watu wazima.
Chanzo
kiliendelea kuweka wazi kwamba baada ya kuwaona wenzao wakielea, watoto
hao walipiga kelele jambo lililowashtua walinzi wa hoteli hiyo upande wa
bwawa ambao walifika haraka kuwatoa marehemu wakiwa tayari
wameshafariki dunia huku mtoto mmoja akihangaika kujiokoa.
“Unajua
wale watoto sijui nisemeje? Waliingia mle kwenye bwawa, inaonekana
walizama, hakuna aliyeweza kuja juu, maji yaliwazidi. Walipokata roho
ndipo miili ikaibuka na kuelea, ndipo wenzao wakapiga kelele,” kilisema
chanzo kwa masikitiko makubwa.
UZEMBE WATAJWA
Habari
zaidi zinadai kuwa sababu kubwa iliyosababisha vifo vya watoto wote
watatu ni uzembe uliofanywa na walinzi wa bwawa hilo ambao walidaiwa
kutokuwa makini kuwadhibiti watoto wengi waliokuwa wakiogelea karibu na
bwawa la watu wazima kiasi cha kutoka na kuingia huko.
MAMA WA MTOTO MWENYE BETHIDEI ATUPIWA LAWAMA
Uzembe
mwingine ulitajwa kufanywa na mama wa mtoto aliyekuwa akisherehekea
siku yake ya kuzaliwa aliyetajwa kwa jina la Anita Mboka kwa kuwachukua
watoto wasio wake na kuondoka nao bila kutoa taarifa kwa wazazi wao japo
kuwa mama wa marehemu Janeth Zakaria (9), Devotha Mbutwa alikiri
kupokea taarifa kuwa mwanaye anakwenda kwenye bethidei ya mwenzake beach
(baharini).
Inadaiwa
mama huyo alipinga mwanaye kwenda kuogelea baharini, lakini alipoambiwa
ni hotelini alikubali bila kujua kuwa nako walikuwa wakienda kupiga
mbizi kwenye bwawa na baadaye kupewa taarifa za kifo chake. Marehemu
alizikwa jana, Iringa Vijijini.
TAARIFA ZA MTOTO WA PILI
Kwa upande wao, ndugu wa karibu wa marehemu
Ndimbumi Bahati (9) walisema hawakupata taarifa yoyote kuhusiana na
mzazi huyo kumchukua mtoto huyo, wakadai siku ya tukio, marehemu
alipelekwa na baba yake kula chipsi jirani na alipomaliza, baba
aliondoka akimuahidi kuwa atakaporejea angemchukua kumpeleka
matembezini, lakini jioni akapata taarifa amefariki dunia.
Marehemu alizikwa jana jijini Mbeya.
KUHUSU MTOTO WA TATU
Nao ndugu wa mtoto marehemu Eva
Nicholaus (11) hawakupatikana mara moja kwa kuwa hadi gazeti hili
linaelekea mtamboni hakukuwa na msemaji rasmi wa familia hiyo ambayo
msiba wake ulikuwa Kijitonyama-Mpakani, Dar. Alizikwa jana Makaburi ya
Sinza jijini Dar.
WAZAZI WAVIPOKEA VIFO KWA MTAZAMO TOFAUTI
Inadaiwa baada ya vifo vya watoto hao wa
mtaa mmoja, kuna wazazi walivipokea vifo hivyo kwa mtazamo tofauti
ambapo kwa mujibu wa ndugu wa karibu wa familia ya Ndimbumi, baba wa
mtoto huyo, Bahati Sisala alikuwa amechanganyikiwa kiasi cha kupoteza
fahamu kwa siku nzima.
Naye mama
mzazi wa mtoto Janeth, Devotha yeye alionekana kuzidi kudhoofu hali
yake kwa kuwa alizipokea taarifa za kifo cha mwanaye akiwa anaumwa
(ugonjwa haikujulikana).
KIJITONYAMA YAZIZIMA
Waandishi wetu walishuhudia wakazi wa
Kijitonyama mahali walipokuwa wakiishi watoto hao wakiwa katika majonzi
makubwa ambapo umati uligawanyika kuaga watoto hao.
Msiba wa
marehemu Ndimbumi uliagwa nyumbani Kijitonyama huku mwili wa mtoto
Janeth ukiagwa katika Hospitali ya Mkoa Kutabibu Kinondoni, Mwananyamala
kabla ya miili hiyo kusafirishwa mmoja kuelekea Mbeya na mwingine
mkoani Iringa.
WANAFUNZI WAMLILIA MWENZAO MSIBANI
Wanafunzi wa Shule ya Msingi Kijitonyama
ambao walikuwa wakisoma na Ndimbumi walifika katika msiba huo na
kusikitisha waombolezaji waliohudhuria msibani hapo baada ya kuangua
vilio jambo lililoongeza simanzi. Marehemu alikuwa akisoma darasa la
nne.
MWENYEKITI, AFISA ELIMU NA KIONGOZI WA DINI WANENA
Kwa upande mwingine Mwenyekiti wa
Mtaa wa Kijitonyama, Alhaus Magoha alisema amesikitishwa sana na vifo
hivyo vilivyotokea ndani ya mtaa wake na kuongeza kuwa hilo ni pigo
kubwa.
Naye
Afisa Elimu wa Kijitonyama, Alexandrina Kahando na Katekista wa Kanisa
Katoliki Parokia ya Mtakatifu Maximilian Kolbe, Mwenge jijini Dar, John
Adolf walifika msibani hapo kuwafariji wazazi wa mtoto Ndimbumi ambao
walikuwa wameishiwa nguvu kutokana na kumpoteza mtoto wao mpendwa.
HOTELI YAGHARAMIA USAFIRI
Habari zilizopatikana wakati gazeti hili
linakwenda mitamboni zilisema kuwa, uongozi wa Hoteli ya Landmark ndiyo
uliojitolea kubeba jukumu la kuisafirisha miili ya Ndimbumi na Janet.
Juzi waandishi wetu walifika kwenye hoteli
hiyo kwa lengo ka kuzungumza na uongozi lakini waliambiwa kuwa viongozi
wote walikuwa kwenye vikao.
0 comments: