Rais Kikwete atoa msamaha kwa wafungwa 3,967 ikiwa ni sehemu ya maadhimisho miaka 50 ya Muungano wa Tanzania
RAIS Jakaya Kikwete, ametoa msamaha kwa wafungwa 3,967 ikiwa ni sehemu ya maadhimisho miaka 50 ya Muungano wa Tanzania.
Kwa
mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari Dar es Salaam jana
na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe, Rais ametoa
msamaha kwa wafungwa kwa kutumia madaraka aliyopewa chini ya ibara ya 45
(1) (d) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Pia
Rais Kikwete amepunguzia wafungwa wote moja ya sita ya vifungo vyao
zaidi ya punguzo la kawaida linalotolewa chini ya kifungu 49 (1) cha
Sheria ya Magereza sura ya 58 isipokuwa wafungwa walioorodheshwa katika
Ibara ya 2(1-xviii).
Kwa
mujibu wa taarifa hiyo wafungwa watakaopata msamaha huo ni wale wenye
magonjwa ya Ukimwi, kifua kikuu na kansa, wazee kuanzia umri wa miaka 70
na zaidi ambao wamethibitishwa na jopo la waganga chini ya uenyekiti wa
mganga mkuu wa mkoa au wilaya.
Alisema
wafungwa wengine ni wale wenye ulemavu wa mwili na akili ambao pia
wamethibitishwa na jopo la waganga chini Uenyekiti wa mganga mkuu wa
mkoa au wilaya wakiwemo pia wafungwa wanawake walioingia na ujauzito
gerezani na wale wenye watoto wanaonyonya na wasionyonya walioingia nao
gerezani.
Msamaha
huo hautawahusu wafungwa waliohukumiwa kunyongwa,wanaotumikia kifungo
cha maisha gerezani,wafungwa wa kupokea na kutoa rushwa,unyang'anyi na
unyang'anyi wa kutumia silaha,wafungwa waliopatikana na silaha au
risasi.
Wengi ambao hawahusiki na msamaha huo ni wafungwa wanaotumikia vifungo
kwa kulawiti,kunajisi na kubaka.
"Mbali
na wafungwa hao, lakini wengine ni wale waliohukumiwa adhabu ya kifo na
adhabu hiyo kubadilishwa kuwa kifungo cha maisha au kifungo gerezani na
wale wote waliofungwa kwa makosa ya kujihusisha na biashara ya dawa za
kulevya," alisema Chikawe.
Chikawe
aliongeza kuwa, wafungwa wengine ambao hawahusiki na msamaha huo ni
wale waliofungwa kwa makosa ya wizi wa magari kwa kutumia
silaha,waliotoroka au waliojaribu kutoroka wakiwa chini ya ulinzi halali
ambao wanatumikia kifungo hicho gerezani na wale waliopatikana na hatia
kwa kutumia madaraka yao vibaya.
Aliwataja
wengi kuwa ni wafungwa wanaotumikia kifungo kwa kosa la kufanya
biashara haramu ya binadamu,nyara za Serikali,ubadhirifu wa fedha za
Serikali.
Wengine ni wafungwa waliopata msamaha na Rais ambao bado wapo gerezani
kutumia sehemu ya kifungo kilichobaki.
Wengine
ambao wataendelea kutumikia adhabu zao ni wale waliofungwa kwa kuwapa
mimba wanafunzi wa shule za msingi na Sekondari na ambao walitenda kosa
hilo wakiwa na umri wa miaka 18 na kuendelea, wafungwa wanaotumikia
kifungo chini ya sheria ya Bodi ya Parole (Act. No.25/1994) na sheria ya
Huduma kwa Jamii (Act.No.6/2002. )
Kundi
la Mwisho ambalo halitahusika na msamaha huo ni wale waliopata msamaha
wa 1/6 ya vifungo vyao zaidi ya punguzo la Kawaida lililotolewa chini ya
kifungu cha 49(1) cha sheria ya Magereza sura ya 58 na bado wafungwa
hao wanatumikia kifungo kilichobaki.
0 comments: