MWELEKEO MPYA BUNGENI, PINDA ATOA HOJA KUTULIZA HALI YA HEWA
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akijibu maswali ya papo kwa hapo Bungeni, mjini Dodoma jana. Picha na Edwin Mjwahuzi
Dodoma. Waziri
Mkuu, Mizengo Pinda jana alifanikiwa kutuliza hali ya hewa bungeni
baada ya kutoa mapendekezo yaliyoungwa mkono na pande zote zilizokuwa
zinavutana kuhusu kupitisha baadhi ya vifungu vya Kanuni za Bunge la
Katiba.
Katika
mapendekezo yake yaliyoungwa mkono na Naibu Katibu Mkuu wa CCM
-Zanzibar, Vuai Ali Vuai, Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba na
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, Pinda alisema: “Nataka kuwaomba
wenzangu wote kwenye maeneo hayo (yenye malumbano) tukiwa tunayapitia
kama hatutaelewana tuyaache kwa muda na kumwomba Mwenyekiti aunde timu
ya watu wazima na wenye busara wajaribu kuyatazama. “Tujadiliane,
tushindane kwa lugha za staha, tusitumie lugha inayoweza kukasirisha.
Isiwe mimi nimesema, mimi nimesema...”
Pinda alilazimika kuingilia kati baada ya kutokea mgawanyiko mkubwa wa namna ya kupiga kura kupitisha vifungu vya rasimu.
Akiunga
mkono ushauri huo, Mbowe alisema Bunge limejaa hisia za hofu ndani na
nje, jambo ambalo linatia wasiwasi wa kupatikana kwa Katiba Mpya.
Alisema iwapo wajumbe watashirikiana na kuweka kando masilahi ya vyama,
idadi yao katika makundi, Katiba inaweza kupatikana.
Vuai
alionya kuhusu matumizi ya lugha za kuudhi huku Profesa Lipumba
akiwataka wajumbe kuzingatia masilahi ya Taifa kama alivyoagiza Rais
Jakaya Kikwete na kutengeneza Katiba ya Watanzania wote bila ya kujali
masilahi binafsi.
Upigaji kura bungeni vita
Awali,
mjadala wa utaratibu wa upigaji kura katika Bunge hilo ulichukua sura
mpya baada ya kudaiwa kuwapo ushawishi unaohusisha utoaji wa bahasha ili
kutaka kuungwa mkono katika misimamo inayokinzana.
Habari
zilizopatikana zilidai kuwa watuhumiwa katika sakata hilo ni baadhi ya
wajumbe ambao ni mawaziri na mbunge mmoja wa CCM. Vigogo hao wanadaiwa
kuwashawishi wajumbe ambao hawatokani na vyama vya siasa ili kupitisha
agenda ya kura ya wazi kirahisi.
Akiandika
kwenye ukurasa wake wa Facebook, Mjumbe wa Bunge hilo, Julius Mtatiro
ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa CUF, alisema: “Jaribio la kuzuia kura
ya siri limechukua njia za aibu, baada ya CCM kutumia fedha kushawishi
wajumbe.”
Katika
ujumbe huo ambao alikiri kuuandika, Mtatiro aliwataja wajumbe watatu
ambao ni mawaziri kuwa waliwakaribisha wajumbe kwenye makazi yao na
“kuwaandalia chakula cha kutosha, vinywaji vya kutosha na viburudisho
vingine, huku wakipewa bahasha za nauli baada ya vikao hivyo vya siri.”
Mmoja wa waliotajwa ni Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe
aliyedaiwa kuwaalika wawakilishi wa wafugaji na kuwapa chakuka na
bahasha.
Akijibu
tuhuma hizo, pamoja na kukiri kuwakaribisha baadhi ya wajumbe na kula
nao chakula, alikana tuhuma za kuwahonga ili waunge mkono msimamo wa
chama hicho. Alisema Mtatiro amemdhalilisha, hivyo anawasiliana na
mwanasheria wake ili kumfikisha mahakamani.
“Siwezi
kumuacha hivihivi Mtatiro, lazima nichukue hatua. Hawa niliwaalika kama
marafiki tu, tukala wote chakula. Mbona hata kesho nimealikwa na Kajubi
Mukajanga (Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania), hivi nikienda
kukutana naye ndiyo atakuwa amenipa rushwa?”
Waziri
mwingine ambaye jina lake linahifadhiwa kwa sababu hakupatikana kujibu
tuhuma zake anadaiwa kuwaalika wawakilishi wa vyuo vya elimu ya juu,
huku mbunge mmoja pia akidaiwa kuwaita wafugaji.
Kulikuwa
na mgawanyiko wa wazi katika kanuni hiyo ya upigaji kura, CCM kikitaka
kuungwa mkono kwa utaratibu wa kupiga kura za wazi huku wapinzani
wakitaka za siri kama zilivyokuwa zimependekezwa na Kamati ya Kumshauri
Mwenyekiti wa Muda kuhusu Kanuni.
Akizungumzia
suala hilo, Mjumbe wa Bunge hilo, Makersia Jibubu alisema: “Sikutarajia
haya. Nilichojua, tungefika wiki ya kwanza tukapitisha kanuni na baada
ya hapo tukaendelea na mijadala. Lakini kinachoonekana ni mivutano ya
wanasiasa na kibaya zaidi wote wanalenga kundi la wajumbe wateule wa
Rais.”
Alisema
alianza kuwa na wasiwasi kuhusu Bunge hilo, mara tu alipofika na kundi
lake kuitwa na moja ya vyama vya siasa kufanya mazungumzo kwa lengo la
kutaka ushawishi wao.
“Makundi
yote yaliyoteuliwa na Rais yaliitwa na vyama vya siasa. Wakaandaa
mikutano kwa chakula na vinywaji, halafu wakaanza kueleza sera zao.
Nikasema sasa hii ni kwa faida ya nani?”
Mkutano wa CCM
CCM
kilifanya mkutano wa wajumbe wake juzi usiku chini ya Makamu wa Pili wa
Rais wa Zanzibar, Balozi Ali Seif Idd. Pamoja na mambo mengine,
kinadaiwa kutoa msimamo kuwalazimisha wajumbe wake kuunga mkono kura ya
wazi.
Chama
hicho kilitumia takriban muda wa saa tatu kuwafunda wajumbe hao ili
kuhakikisha kuwa wanatetea utaratibu huo. Mkutano huo ulianza saa 2:15
hadi saa 5:00 usiku.
Habari kutoka ndani ya kikao hicho, zilidokeza kuwa ajenda kuu ilikuwa ni kupitia rasimu ya kanuni.
Mjumbe
mmoja alisema: “Inavyoonekana sasa suala la kupiga kura ya wazi ni amri
na halina tena mjadala, lakini litaleta matatizo makubwa mbele ya
safari… yetu macho.
“Mle ndani sisi wengine tuliamua kunyamaza kimya, maana hata unaposimama na kuchangia bado watu wanakuona kama ni msaliti.”
Wakati
wa semina ya wajumbe kuhusu rasimu ya kanuni, wajumbe wawili kutoka
CCM, Ester Bulaya na Profesa Juma Kapuya waliweka wazi kuwa wanaunga
mkono kura za siri, huku Anna Kilango akisema suala la ama kupigwa kura
ya wazi au ya siri liamuliwe kwa kura ya siri kwa kuwa limezua mvutano.
Kikao cha Ukawa
Katika
hatua nyingine, wapinzani na wajumbe wa makundi mengine ya kijamii
chini ya Umoja wao wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), walikutana katika
Ukumbi wa Pius Msekwa na kuweka msimamo wa kupinga kura ya wazi kwa
nguvu na gharama zozote.
Mmoja
wa wajumbe wake, John Mnyika alisema uamuzi mwafaka ni kura ya siri
kuamua vifungu mbalimbali vilivyomo katika Rasimu ya Katiba. Mjumbe
Tundu Lissu alisema: “Hatutakubali zipigwe kura za wazi, sisi bado
tumesimamia palepale.”
Sitta na Suluhu wapitishwa
Habari
zilizopatikana jana jioni zinasema wajumbe wa Bunge hilo wa CCM
walikutana na kuwapitisha Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Samuel Sitta na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano),
Samia Suluhu Hassan kuwania nafasi za uenyekiti na makamu mwenyekiti’.
0 comments: